Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi,
Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama
|
Serikali imeamua wakati wowote kuanzia mwezi huu kuanza
kukagua vibali vya ajira za wageni nchini.
Hatua hiyo inafuatia baada ya siku 14 kumalizika
zilizotolewa na serikali katika tangazo la utolewaji wa vibali vya kazi kwa
wageni nchini.
Tangazo hilo lilisainiwa Desemba 14, mwaka huu na Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye
Ulemavu), Jenista Mhagama (pichani).
Katika tangazo hilo, Waziri Mhagama aliwataka waajiri
wote nchini kwa muda wa siku hizo wawe wametekeleza matakwa ya Sheria ya
Kuratibu Ajira za Wageni nchini Na. 1 ya mwaka 2015.
“Katika taarifa tuliyoitoa mwezi huu, uliwajulisha
waajiri wote wenye waajiri wa kigeni ambao wana vibali vya kazi za muda (Carry
on Temporary Assignment) na wale wote wasiokuwa na vibali vya ajira
vilivyotolewa na Kamishna wa Kazi nchini, kuwa wanatenda kosa. Kamishna wa Kazi
amepewa mamlaka kutoa vibali vya ajira kwa wageni wanaotaka kufanya kazi
nchini. Hivyo hakuna mamlaka nyingine yoyote inayoruhusiwa kutoa vibali vya ajira
kwa wageni,” alisema Mhagama.
Aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati
akizungumza na kikosi maalum kitakachoendesha operasheni hiyo chenye wajumbe
kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uhamiaji na Wakala wa Usalama na Afya
mahali pa kazi (OSHA), ikiwa lengo ni kufuatilia kama agizo lililotolewa na
serikalil imefuatwa na kuhakikisha taratibu zinazopaswa kufuatwa katika utoaji
wa vibali vya ajira zinazingatiwa.
“Serikali ilitoa siku 14 kwa waajiri wote wawe
wametekeleza matakwa ya Sheria Na. 1 ya mwaka 2015 vinginevyo hatua kali za
kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” alisitiza Mhagama.
Mwezi Machi, mwaka huu Bunge la 10 la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania lilipitisha Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni chini Na. 1 ya mwaka
2015 (The Non-Citizens (Employment Regulation) Act)).
Sheria ilianza kutumika rasmi tangu Septemba 15, mwaka
huu.
Sheria hiyo inaanzisha Mamlaka moja ya utoaji wa vibali
vya ajira kwa wageni na mamlaka hiyo ni Kamishna wa Kazi.
No comments
Post a Comment