Friday, 8 May 2015

JK awasafisha mawaziri waliotimuliwa na Bunge

Balozi Sefue asema walioonekana hawana hatia pia wamo Profesa Muhongo, Maswi Tume imeona wote hawakuhusika na ukiukwaji wa haki za binada... thumbnail 1 summary
  • Balozi Sefue asema walioonekana hawana hatia pia wamo Profesa Muhongo, Maswi
  • Tume imeona wote hawakuhusika na ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa Operesheni Tokomeza na waliwajibika kisiasa. Kwa hiyo hakuna hatua zozote zinazoweza kuchukuliwa dhidi yao
Baada ya kimya cha muda mrefu, hatimaye Ikulu imewasafisha mawaziri wanne walioshinikizwa na Bunge kujiuzulu kutokana na kuhusishwa na sakata la Operesheni Tokomeza Ujangili, Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini waliohusishwa na sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.
Waliotangazwa kuwa safi ni Emmanuel Nchimbi, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Shamsi Vuai Nahodha, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Wawili hao wanatajwa kwenye kinyang’anyiro cha urais kwa tiketi ya CCM ingawa hawajatangaza nia.
Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki na aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, David Mathayo.
Hali kadhalika, Profesa Sopster Muhongo aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini ametangazwa kuwa safi pamoja na katibu mkuu wa wizara hiyo, Eliackim Maswi, ambao walihusishwa na sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh306 bilioni kutoka akaunti ya Tegeta Escrow.
Uamuzi wa Ikulu kuwaondolea doa hilo mawaziri hao wanne umetokana na ripoti ya Tume iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete kuchunguza tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo iliyolenga kuondoa ujangili kwenye hifadhi za Taifa, lakini ikaishia kuua wananchi, kutesa na kupora mali zao.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue aliwaambia wanahabari kuwa tume iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete ilijiridhisha kuwa mawaziri hao  waliwajibika kisiasa na hawakuhusika moja kwa moja na vitendo hivyo na hakuna hatua inayostahili kuchukuliwa dhidi yao.
Rais Kikwete aliunda tume hiyo Mei mosi mwaka jana kuchunguza malalamiko yaliyotokana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Operesheni hiyo ilibuniwa na Wizara ya Maliasili na Utali kwa lengo  la kupambana na ujangili ambao ulikithiri hadi  taasisi za kimataifa kuingilia kati. Hata hivyo ilisitishwa Novemba Mosi, 2013 ili kupisha uchunguzi wa malalamiko yaliyojitokeza.
Tume hiyo ilikuwa na makamishna watatu, ikiwa chini ya uenyekiti wa Balozi Hamisi Msumi, Jaji Stephen Erenst, Jaji Vicent Kitubio na Frederick  Lema ambaye alikuwa katibu.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari, Balozi Sefue alisema licha ya  mawaziri hao kuonekana wasafi, bado tume ilibaini ukiukwaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu  katika utekelezaji wa operesheni hiyo. mwananchi

No comments

Post a Comment