Tuesday, 5 May 2015

Kamati ya Bunge yaikataa bajeti Maliasili na Utalii

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu, ya Maliasili na Utalii, James Lembeli KAMA... thumbnail 1 summary


KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Maliasili na Utalii jana ilikataa kujadili bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii huku ikiwataka Waziri na watendaji wake kuondoka ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dar es Salaam ambako walikuwa wakutane kwa majadiliano.
Sababu kubwa imetajwa ni wizara hiyo kushindwa kutekeleza maagizo yaliyotolewa na kamati hiyo, ikiwemo kukaidi amri ya Mahakama Kuu ya kutaka kuanza mara moja utekelezaji wa tozo mpya kwenye Hifadhi za Taifa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu, ya Maliasili na Utalii, James Lembeli alitoa uamuzi huo jana jijini Dar es Salaam wakati kamati hiyo ilipokutana na wizara hiyo chini ya Waziri wake Lazaro Nyalandu ambaye alikiri kuwapo kwa tatizo katika ripoti huku akiahidi kufanyia kazi.
“Hatuwezi kupitia bajeti hii, kwa sababu maagizo tuliyotoa awali hayajatekelezwa, sasa tuna uhakika gani kama tukipitia hii bajeti yao ya mwaka 2015/16, watakwenda kutekeleza tutakachoagiza?” Alihoji Lembeli.
Alisema kimsingi, wizara hiyo imekwenda kinyume na makubaliano yao na kwamba ni vyema wizara hiyo ikaenda kujipanga na kufanya marekebisho ya maagizo yaliyotolewa kisha kurejea kujadili bajeti hiyo.
Lembeli aliyataja maagizo yaliyotolewa na kamati hiyo kuwa ni pamoja na utaratibu wa kiingilio kwenye hifadhi, ambapo tozo iliyotakiwa ni kila mtalii anapoingia anachajiwa kiingilio na akitoka na kutaka kuingia tena ni lazima alipe.
Alisema jambo hilo halizingatiwi na kwamba serikali imeingilia na kufuta tozo hiyo ambayo hivi sasa watalii wanaingia na kutoka na kisha kuingia tena bila kulipa jambo linalokosesha hifadhi mapato.
Kuhusu amri ya Mahakama, Kamati ilimtaka atekeleze agizo lililotolewa na Mahakama kuhusu utekelezaji wa kutoa tangazo kwenye gazeti la serikali kuhusu tozo mpya za kodi za utalii ambapo Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilitoa agizo hilo Septemba mwaka jana na kutaka utekelezaji wake uanzi mara moja.
Lembeli alisema tangu kutolewa na agizo hilo imeshapita miezi kadhaa utekelezaji wake haujafanywa na waziri, jambo ambalo linaokosesha mapato ya Sh bilioni 80 kwa mwaka, Mamlaka ya Hifadhi Tanzania (Tanapa).
Akizungumzia agizo jingine, alisema ni mgogoro wa mipaka kwenye Hifadhi ya Taifa ya Saadan ambapo kamati iliagiza kuwa mipaka ya hifadhi hiyo ibaki kama ilivyokuwa tangu awali, lakini kinyume chake, wizara imemega sehemu ya ardhi na kuitafutia hati miliki.
Waziri Nyalandu alikiri kuwepo na matatizo kwenye maagizo ya ripoti hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi hiyo jana na wataalamu wa wizara hiyo ili wahakikishe wanatatua changamoto hizo, na leo wanaweza kutoa ripoti hiyo ili kamati ijadili bajeti yao. source habari leo, may 5, 2015

No comments

Post a Comment