KUTOKANA na kushamiri kwa matukio yenye viashiria vya kigaidi nchini,
Kanisa Kuu Katoliki Jimbo la Dodoma limeanzisha utaratibu wa kukagua
watu wote wanaoingia katika ibada kwa kutumia kifaa maalumu cha kugundua
silaha au kifaa chochote hatarishi na vile vya mlipuko.
Aidha, wito umetolewa kwa waumini wa madhehebu ya Kikatoliki
wanaohudhuria ibada zao kwenye Kanisa hilo, kuchukua tahadhari zote
kukabiliana na suala la tishio la usalama kwa matukio ya kigaidi,
yanayoweza kujitokeza kanisani hapo, kutokana na mkusanyiko mkubwa wa
watu wanaohudhuria ibada siku za Jumapili.
Paroko wa Kanisa hilo, Padri Sebastian
Mwaja alitoa wito huo jana wakati akiendesha ibada za kawaida za Jumapili.
Alisema kanisa hilo limeanzisha utaratibu wa kuwakagua watu wote
wanaoingia katika ibada hizo kwa kutumia kifaa maalumu cha kugundua
silaha au kifaa chochote hatarishi na vile vya mlipuko.
Padri Mwaja alisema idadi ya waumini imeongezeka ghafla hususani
baada ya Jimbo la Dodoma kumpata na kumsimika rasmi Askofu Mkuu mpya wa
Jimbo la Dodoma.
“Pia mji wetu kuwa na desturi ya kupokea wageni wengi wa kiserikali,
ni wazi hatuwezi kujisahau na kuacha suala la usalama wa waumini wetu,”
alisema paroko huyo.
Alitaja baadhi ya hatua zilizoanza kuchukuliwa kukabiliana na
matishio ya vitendo vya kigaidi kuwa ni pamoja na kuundwa kwa kamati ya
ulinzi ya kanisa hilo ijulikanayo kwa kifupi “KAUKA”, ambapo baadhi ya
taratibu za awali tayari zimeshawekwa na kamati hiyo, ikiwamo tahadhari
kwa waumini wote kuhakikisha anamtambua jirani yake aliyekaa naye
kanisani, na kama atamtilia shaka yoyote, atoe taarifa mapema katika
kamati hiyo.
Hatua nyingine iliyochukuliwa ni pamoja na kuhakikisha kila muumini
anayeingia kanisani hapo anakaguliwa ndipo aingie ndani ya kanisa na pia
magari yote pamoja na pikipiki kuachwa nje ya ua wa parokia hiyo katika
eneo maalumu lililoandaliwa ili kudhibiti usalama.
Paroko huyo ametaja pia changamoto iliyojitokeza wakati wa kutekeleza
ulinzi huo, ikiwemo upungufu wa vifaa vya ukaguzi ambapo hadi sasa kipo
kifaa kimoja tu kinachotumika kwenye lango (geti) moja na mengine
kubakia yamefungwa.
Alieleza kifaa hicho kina thamani ya Sh 750,000 na vinatakiwa
takribani vinne ili vitumike kwa wakati mmoja wakati wa ibada za
asubuhi.
Pia, ametoa wito kwa waumini wenye uwezo wa kutoa ufadhili wa vifaa
hivyo kama ilivyofanyika kwa kilichopo sasa, kufanya hivyo mapema ili
waumini wawe na uhakika wa usalama wao wanapokuwa katika ibada.
Pameonekana msururu mrefu wa waumini wanaotaka kuwahi kuingia katika
ibada za asubuhi siku za Jumapili, lakini huchelewa kutokana na ukosefu
wa vifaa vya kutosha.
Kwa upande mwingine, kampuni moja inayojihusisha na ukusanyaji wa
kodi ya kuegesha magari hapa Dodoma, nayo inaonekana kufurahia mpango
huo wa magari kutoingia ndani ya kanisa hilo, na wao kukusanya kodi zao
za maegesho nyakati za asubuhi.
Waumini wengi wameonesha kuridhishwa na hatua hiyo ya kamati ya
ulinzi, ikielezwa Dodoma iko hatarini zaidi kutokana ujio wa wageni
wengi katika mji huo mkuu wa Tanzania, wakitolea mfano Bunge la Bajeti
linalotarajiwa kuanza wiki ijayo.
Aidha, kushikiliwa kwa mwanafunzi wa kitanzania anayetajwa
kujihusisha na ugaidi katika Chuo Kikuu cha Garisa nchini Kenya
kumeongeza hofu, kwani alikuwa akisoma shule ya sekondari Bihawana, nje
kidogo ya mji huu.
Mbali na Dodoma, viashiria vya matukio ya kigaidi vimejitokeza katika
mkoa jirani wa Morogoro, ambako bomu lililotupwa na kijana ambaye
hajafahamika, limejeruhi vibaya watu watano. Tukio hilo la mwishoni mwa
wiki lilitokea kijiji cha Msolwa kata ya Sanje wilaya ya Kilombero.
Sunday, 3 May 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments
Post a Comment