Sunday, 10 May 2015

Kikwete aita marais EAC kuijadili Burundi

RAIS Jakaya Kikwete ameitisha mkutano wa wakuu wenzake wa nchi tano za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili kujadili hali ya Burundi. Amei... thumbnail 1 summary
Rais Jakaya KikweteRAIS Jakaya Kikwete ameitisha mkutano wa wakuu wenzake wa nchi tano za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili kujadili hali ya Burundi.
Ameitisha mkutano huo wakati Burundi ikiripotiwa kuwa katika vurugu zinazotishia hali ya usalama, hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi ujao.
Rais Kikwete amechukua uamuzi huo kwa wadhifa alionao wa Mwenyekiti wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Alitangaza kuitisha mkutano huo wakati alipozungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN), kuwaelezea matokeo ya mkutano wa wiki moja wa Jopo la Watu Mashuhuri Duniani, linaloangalia jinsi dunia inavyoweza kukabiliana na majanga ya kiafya katika siku zijazo kufuatia balaa la ugonjwa wa ebola katika Afrika Magharibi.
Rais Kikwete na wana-Jopo wenzake walizungumza na wanahabari juzi jijini New York, baada ya kuwa wamemaliza kikao cha kwanza cha Jopo lao lililoteuliwa na Katibu Mkuu wa UN, Ban Kimoon, Aprili 2, mwaka huu, 2015, kupendekeza jinsi dunia inavyoweza kukabiliana na majanga ya kiafya, na hasa ya magonjwa ya mlipuko, katika siku zijazo kufuatia balaa na athari za ugonjwa wa ebola katika Afrika Magharibi.
Ugonjwa wa ebola umeua watu karibu 10,000 katika kipindi kifupi katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone. Ugonjwa huo ulijitokeza kwa mara ya kwanza mwaka 1976, karibu miaka 40 iliyopita katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Mpaka sasa ugonjwa huo hauna dawa inayojulikana dhahiri wala chanjo. Katika maswali yaliyofuatia maelezo yake na ya wanajopo wenzake kuhusu kazi yao ya wiki moja, Rais Kikwete aliulizwa kuhusu hali ilivyo katika Burundi na Tanzania, kama jirani inachukua hatua gani kukabiliana na hali hiyo katika nchi jirani.
Rais Kikwete alisema baada ya mawaziri wa nchi za nje wa Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda kuwa wametembelea Burundi majuzi, kwa maelekezo yake, na kumaliza ziara yao kwa kujionea hali ilivyo katika nchi hiyo, ameamua kuitisha Mkutano wa Wakuu wa Nchi za EAC jijini Dar es Salaam, ambako mawaziri hao watatoa ripoti yao ili ijadiliwe.
“Tumekubaliana kuwa sisi ndani ya EAC – Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi yenyewe tukutane Dar es Salaam, Jumatano ijayo, Mei 13 (keshokutwa), ili tujadiliane jinsi gani ya kuwasaidia ndugu zetu wa Burundi kuandaa uchaguzi wao kwa mafanikio, wakihakikisha kuwa nchi yao inabakia na umoja, utulivu, usalama na amani bila misukosuko isiyokuwa na sababu,” Rais Kikwete aliwaambia waandishi hao wa habari.
Rais Kikwete aliongeza: “Baada ya hapo, tutaweza sasa kuwaelezea nyie waandishi wa habari kuhusu msimamo wa EAC na hata msimamo wa Tanzania kuhusu Burundi – tuwe na subira na tunaamini kuwa Burundi itaendelea kuwa ya utulivu na amani.”
Katika siku za karibuni, kumekuwepo na hali ya mjadala mkali kuhusu maana halisi hasa ya Katiba ya Burundi, hususani katika kipengele kinachohusu vipindi vya kutumikia Urais.
Baadhi wamekuwa wanadai kuwa kwa kutumikia miaka 10, Rais wa sasa, Pierre Nkurunziza amekamilisha mahitaji ya kikatiba. Wengine wanasema kuwa bado anayo haki ya kugombea kwa kipindi kimoja zaidi, kwa sababu Rais amechaguliwa mara moja tu na wananchi.
Chama chake cha CNDDFDD kimempitisha tena kuwa mgombea urais na wiki iliyopita Mahakama ya Katiba, ilisema Rais Nkurunziza anayo haki ya Kikatiba kuwania nafasi hiyo kwa mara nyingine.
Hali ilivyo Burundi Kwa ujumla, wapinzani wa Rais Nkurunziza wameendelea kufanya maandamano bila kikomo ya kumpinga kuwania urais kwa awamu ya tatu katika uchaguzi mkuu wa Juni.
Kutokana na maandamano hayo yaliyodumu kwa wiki mbili, hadi sasa watu 18 wameuawa tangu Rais Nkurunziza atangaze nia yake hiyo, huku maelfu wakiimbia nchi yao kwenda kujisalimisha katika nchi jirani.
Kwa upande wa Tanzania, zaidi ya Warundi 15,000 wameripotiwa kuingia wakipitia mpaka wa kijiji cha Kagunga Kigoma Vijijini, ambako baada ya kupokewa wanapelekwa moja kwa moja katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu wilayani Kasulu.
Wakimbizi wengine wanaingia nchini kupitia mpaka wa Ngara na Misenyi, ambako hata hivyo wametakiwa kurejea makwao baada ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongela kusema kwa sasa hakuna maandalizi yaliyofanywa kuwapokea wageni hao.

No comments

Post a Comment