Chifu wa Wasafwa anayetambulika kwa jina la Mwene. Stori: Gabriel Ng’osha CHIFU wa Wasafwa anayetambulika kwa jina la Mwene (...
22:54
Chifu
wa Wasafwa anayetambulika kwa jina la Mwene. Stori: Gabriel Ng’osha
CHIFU wa Wasafwa anayetambulika kwa jina la Mwene (kwa Kisafwa), Rocketi
Mwanshinga hajawahi kunyoa nywele kwa miaka saba tangu amekuwa kiongozi
wa kimila wa kabila hilo.
Chifu Mwanshinga aliyeanza kutawala
tangu mwaka 2008, hajawahi kunyoa nywele zake kwa miaka saba sasa na
anazitumia kwa shughuli za matambiko kimila huku zikibadilika muonekano
na kuwa kama rasta.Inadaiwa kuwa nywele za chifu huyo ni nadra sana
kuziona kwa sababu ni sehemu ya tambiko lao na muda mwingi huwa
zimefunikwa kwa kilemba maalumu na huondoa kilemba hicho panapokuwa na
sherehe za kimila.
Akizungumza
kwa njia ya simu na Uwazi juzi, Chifu Mwanshinga alisema:“Mimi ni chifu
mkuu siruhusiwi kunyoa nywele zangu mpaka nakwenda kaburini kwa sababu
zinasaidia sana katika matambiko ya Kisafwa, ambayo huwa tunayafanya
katika Msitu wa Ianjo kwa sababu msitu ni mzito na mnene na mimi nywele
zangu zinatakiwa kuwa kama msitu huo.”
Wasafwa ni moja ya kabila
linalopatikana mkoani Mbeya, ambalo bado linaongozwa kwa kukuza
utamaduni na mila zake ikiwemo ile ya utawala wa kichifu, kufanya
matambiko, kwa ajili ya kuomba mvua, amani, uchaguzi, biashara na mambo
mengine na moja ya shughuli hiyo iliwahi kuhudhuriwa na Mbunge wa Mbeya
Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’.
Sherehe za Wasafwa nyingi
hufanyika katika misitu, moja ya msitu ambao umekuwa ukitumika kwa
matambiko hayo ni ule wa Ianjo unaopatikana maeneo ya Igawilo na
unalindwa kijadi huku ukiaminika kuwa na maajabu.Miongoni mwa masharti
katika msitu huo ni kutopiga picha baadhi ya maeneo, kutokuokota kuni,
kukata miti na mengineyo.
No comments
Post a Comment