Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hosea alisema jana kuwa mafunzo hayo yanayofanyika katika taasisi ya Mafunzo ya Vitendo kwa Wanasheria, yanalenga kuwajengea uwezo wanasheria wanaohusika na kesi za rushwa kutambua namna ambavyo ushahidi wa mazingira ulivyo muhimu katika kesi hizo.
“Kesi za rushwa nyingi ushahidi wake muhimu ni wa kimazingira, lakini katika hali ya kawaida mahakama zimekuwa hazitilii maanani ushahidi huo hali ambayo imechangia watuhumiwa wengi wa kesi za rushwa kuachiwa huru,” alisema.
Alisema kutokana na watuhumiwa wengi wa makosa ya kifisadi kuachiwa huru kwa kukosekana ushahidi, Dk Hosea alisema kuna umuhimu wa majaji na mahakimu kupewa mafunzo ya kutambua mfumo wa kesi za makosa ya rushwa na jinsi ilivyo muhimu kwa ushahidi wa kimazingira.
Alitoa mfano kuwa mazingira yenyewe yanaweza kuwa mtu katumiwa pesa kutumia simu ya mkononi au mpelelezi anaweza kuwa amerekodi mazungumzo ya mtoaji na mpokeaji rushwa, “Sasa unakuta mahakimu wetu na waendesha mashitaka wanakuwa hawako pamoja katika kuamini ushahidi huo na kesi inatupiliwa mbali.”
Dk Hosea alionesha kusikitishwa kuona namna ambavyo mahakama nchini zinavyotoa nafasi ndogo kwa ushahidi wa mazingira na akaongeza kuwa ndio maana wameona kuna umuhimu wa wataalamu kutoka nje kuja nchini kutoa mafunzo ili kuwajengea uwezo mahakimu na majaji juu ya umuhimu wa ushahidi huo.
Mafunzo hayo yanatolewa na wataalamu kutoka Shule ya Sheria ya Northwestern ya Marekani, Profesa Thomas Geraghty na wanasheria kutoka Chama cha Wanasheria wasio na mipaka ambao kwa siku tano watawanoa wanasheria wa Takukuru na mahakimu namna ya kuwasilisha ushahidi wa makosa ya rushwa.
Dk Hosea alikiri kuwa wananchi wamekuwa wanakatishwa tamaa kutokana na kuona watuhumiwa wa rushwa wanaachiwa huru na mahakama na akasema anaamini kuwa mafunzo hayo yatawajengea uwezo wanasheria wa Takukuru na mahakimu juu ya ushahidi wa makosa ya rushwa.
Naye Jaji Kiongozi Shaaban Lila alisema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo majaji, mahakimu, waendesha mashitaka na wapelelezi wa kesi za rushwa ili kutambua ushahidi unaotakiwa mahakamani ni ule tu ambao unathibitisha makosa.
Alisema kwa sasa ushahidi mwingi unaotolewa na wapelelezi na waendesha mashitaka mahakamani unaweza kuwa mrefu, lakini hauthibitishi makosa yaliyoko mahakamani jambo ambalo limechangia watuhumiwa wa kesi nyingi za rushwa kuachiwa.
“Unakuta shahidi mmoja anatoa ushahidi wake kwa wiki moja, ni kweli kwamba siku zote hizo anatoa ushahidi kuthibitisha kosa lililoko mahakamani? Unaweza kukuta ushahidi uko nje na mwisho wa siku mtuhumiwa anaachiwa,” alisema Jaji Lila.
Alisema iwapo mamlaka hizo mbili zikishirikiana kwa kutoa ushahidi ule tu ambao unathibitisha mashitaka yaliyoko mahakamani hata muda wa kusikiliza kesi unakuwa mfupi kuliko ilivyo sasa.
Alisema mafunzo hayo yatasaidia kuwajengea uwezo wanasheria hao ambao wanahusika na kesi za rushwa. source habari leo, may 5-2015
No comments
Post a Comment