Friday, 8 May 2015

UV-CCM; huyu ndiye Rais tumtakaye.

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umetaja sifa za mgombea urais, anayetakiwa kugombea kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu ... thumbnail 1 summary
Katibu Mkuu wa Taifa UVCCM Taifa, Sixtus Mapunda UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umetaja sifa za mgombea urais, anayetakiwa kugombea kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa Taifa UVCCM Taifa, Sixtus Mapunda alisema “Mbali na sifa 14 za miaka yote tunazozifahamu, sifa kuu kwa mazingira ya siasa za sasa ni CCM kuwa na mgombea anayekijua chama vizuri, ndani na nje.”
Alisema CCM inahitaji mgombea wa aina hiyo, kwa sababu mbali na kwamba ndiye atakayekuwa Rais wa Tanzania, lakini pia atakuwa Mwenyekiti wa CCM wa Taifa.
Alitaja sifa nyingine kuwa ni lazima awe mchapakazi, anayekubalika na kupendwa na watu, mpenda watu, mpenda amani na muungano na asiwe na ubaguzi wowote.
Alisema pamoja na sifa hizo, CCM inahitaji mgombea atakayekubali Tanzania ianze na moja kwa kuwashawishi wananchi wakubali kujifunga mkanda kwa kuanza kufanya mambo machache, lakini yatakayosambaza neema katika maeneo mengine kwa muda mfupi.
“Ni lazima ayapunguze au asitishe matumizi yote yasiyo ya lazima ili kuimarisha matumizi yanayoweza kuongeza tija katika maeneo yanayoweza kufungua neema nyingine,” alisema.
Mapunda alisema CCM inahitaji mgombea ambaye ni rafiki wa vijana, anayezijua changamoto zao na mwenye mipango inayoelezeka ya namna ya kuzishughulikia.
“Zipo changamoto kubwa mbili zinazowakabili vijana wa Tanzania, nazo ni elimu na ajira. Kwa upande wa elimu ni lazima aje na mikakati itakayotoa fursa kwa vijana wengi kupata elimu ya msingi hadi chuo kikuu na kwa upande wa ajira ni lazima aje na mipango itakayowezesha kuzalisha ajira nyingi hasa katika sekta binafsi,” alisema.
Alisema matarajio ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ni kuunda serikali ya awamu ya tano, kwa sababu bado ni chama imara, kinachokubalika na watu na kina idadi kubwa ya wagombea wenye sifa lukuki katika nafasi mbalimbali

No comments

Post a Comment