Askofu Josephat Gwajima
Watoto hao walifariki dunia kutokana na kupigwa na shoti ya umeme wakiwa katika ibada juzi.
Tukio hilo lilitokea wakati watoto hao wakiwa na waumini wengine wakifuatilia ibada ya kufunga ndoa.
Inadaiwa kuwa, watoto hao walipigwa na shoti baada ya kukanyaga
nyaya za umeme wakati wao na waumini wengine walipoamka vitini kwenda
kuwapokea maharusi wakati wakiingia kanisani hapo.
BABA ATILIA SHAKA
Hata hivyo, baba mzazi wa watoto hao, David Oturo, ameonyesha hali
ya wasiwasi na kutokukubalina na mazingira ya vifo vya watoto wake,
Sarah (10), Goodluck (4) na kusema ni vifo vya utatanishi.
Akizungumza jana kuhusiana na vifo hivyo alieleza kuwa, Sarah
alikuwa anasoma Shule ya Msingi Milambo iliyopo Mbezi Juu darasa la nne
na Goodluck alikuwa anasoma chekechea ya Ushindi.
Alisema siku hiyo kulikuwapo na watoto wengi waliokusanyika katika
viwanja vya kanisa hilo, lakini ni watoto wake tu ndiyo waliofikwa na
mauti huo.
“Pale kanisani kulikuwa na watoto wengi na waumini wengine lakini kwanini imetokea kwa watoto wangu tu?” alihoji.
Aliongeza kuwa kabla ya kukutwa na mauti jioni, majira ya mchana,
Sarah aling’atwa na nyuki sehemu ya mguuni waliotokea katika kanisa hilo
ghafla.
Alisema ilipofika jioni ndipo watoto wake peke yao walikanyaga nyaya za umeme zilizokuwa zimepitishwa katika viwanja hivyo.
Oturo alifafanua kuwa nyanya hizo za umeme hazikuwa zimechunika wala hazikuwa na dalili ya kuwa na hitilafu.
“Sehemu yenyewe haikuwa na mchubuko wowote wa waya, wala hakukuwa
na hitilafu yoyote, ilikuwa ni sehemu ambayo inaonekana imetengenezwa na
mtu ambaye ni mtaalam wa masuala ya umeme,” alisema Oturo.
Alisema watoto hao walikuwa na mama yao ambaye ndiye anayekweda nao kila siku ya Jumapili katika ibada.
Oturo aliongeza kuwa, baada ya watoto wake kupigwa na shoti ya
umeme, walipewa huduma ya kwanza na uongozi wa kanisa hilo na kisha
kukimbizwa katika Hospitali ya TMJ.
Akielezea huku akionekana kuwa na huzuni, Oturo alisema baada ya
kufikishwa katika hospitali hiyo, walipelekwa katika hospitali ya
Mwananyamala na ndiko mauti yalipowafikia.
“Sehemu yoyote kunapokuwa na shoti lazima fundi umeme atakuwapo,
lakini kitu cha kushangaza kwa nini imewakuta watoto wangu tu, wakati
kulikuwapo na umati wa watu wengi?” alihoji baba wa watoto hao.
Alisema waliripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi cha Kawe na kuandikiwa RB KW/RB/5374/2015.
Oturo alisema kwa sasa wanasubiri uchunguzi wa Jeshi la Polisi ili miili isafirishwe kuelekea Musoma, mkoani Mara kwa mazishi.
MASHUHUDA WASIMULIA
Baadhi ya mashuhuda waliokuwapo wakati wa tukio hilo, Aida Simon
na Sylvia Gozbert, walieleza kuwa siku ya tukio kulikuwa na harusi
kanisani hapo.
Walisema maharusi walipokuwa wanaingia kanisani, Askofu akawaambia
watoto na waumini kwenda kuwapokea na kuwashangilia maharusi hao.
Walisema ghafla wakati tukio hilo likiendelea ndipo watoto hao walipigwa na shoti ya umeme.
UONGOZI WA KANISA WAZUNGUMZA
Askofu wa Kanisa hilo, Josephat Gwajima, alisema kuwa tukio hilo lilitokea baada ya yeye kuondoka kanisani hapo.
Alisema ni kweli watoto hao walifariki kutokana na shoti ya umeme iliyotokea kanisani hapo.
“Kwa sasa sina taarifa kamili kwa sababu tukio lilitokea baada ya
mimi kuondoka kanisani, lakini ni kweli watoto hao wamefariki na hivi
sasa ninaelekea kanisani ambako nitapata taarifa kamili,” alisema
Gwajima.
KAULI YA POLISI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura,
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. Wambura alilieleza kuwa,
uchunguzi bado unaendelea wa kubaini kama ni kweli tukio hilo
lilisababishwa na kukanyaga nyaya za umeme.
Alisema polisi pia wanachunguza kufahamu kama kuna tukio la
makusudi ama kulikuwa na uzembe wowote uliosababisha kutokea kwa vifo
hivyo.
“Baada ya uchunguzi huo kukamilika, ndipo tutajua ni hatua gani za
kisheria tutakazozichukua kutokana na tukio hilo,” alisema Wambura.
NIPASHE
No comments
Post a Comment