Habari kutoka Korea Kaskazini
zinasema kuwa, Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo, Hyon Yong Chol, ameuawa
baada ya kupatikana na hatia ya kumvunjia heshima kiongozi mkuu wa nchi
hiyo, Kim Jong Un. Habari zaidi zinasema kosa la Waziri huyo wa Ulinzi
ni kusinzia kwenye hafla ya kijeshi iliyokuwa imehudhuriwa na Kim; jambo
lililochukuliwa kuwa ukosefu wa heshima kwa kiongozi wa nchi na hivyo
kutafsiriwa kuwa kosa la uhaini. Hyon Yon Chol ni miongoni mwa maafisa
16 wa ngazi za juu katika serikali ya Pyongyang kunyongwa mwaka huu
pekee kutokana na tuhuma za uhaini.
Kim Jong Un aliingia madarakani mwaka
2011 baada ya kufariki dunia baba yake Kim Jong-ill na tangu wakati huo
amekuwa akiwaondoa watu wanaodhaniwa kuwa ni tishio kwa uongozi wake.
Mwaka 2013 aliamuru kunyongwa mjomba wake, Jang Song Thaek, kutokana na
tuhuma za ufisadi na kuhujumu uchumi wa taifa. Jang Song Thaek alikuwa
miongoni mwa shaksia waliokuwa na ushawishi mkubwa wakati wa uongozi wa
Kim Jong-ill.
Irani swahili radio. mei 13, 2015
No comments
Post a Comment