Tuesday, 5 May 2015

Wizara yakana magazeti




WIZARA ya Nishati na Madini imekanusha habari zilizoandikwa na magazeti ya kila siku ya Nipashe na Tanzania Daima dhidi ya Waziri wa Wizara hiyo, Profesa Sospeter Muhongo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Nishati na Madini na kusambazwa kwa vyombo mbalimbali vya habari nchini, Mei 15, 2014 gazeti la Nipashe toleo nambari 0578116 lilichapisha taarifa yenye kichwa cha habari “Muhongo akaliwa kooni ang’oke” na kudai Waziri Profesa Muhongo amekuwa akilalamikiwa na Watanzania wazawa  kutokana na kauli zake za kuwatukana, kuwabeza na kuwadhalilisha akidai kuwa hawana uwezo wa kushiriki katika biashara ya kuvuna gesi asilia na  mafuta kutokana na kutokuwa na fedha kama mitaji.
Taarifa hiyo pia ilidai kuwa Profesa Muhongo analidhalilisha Taifa kutokana na vitendo vyake vya kugawa madini kwa wageni na kuwaondoa mamilioni ya wazawa kwenye uchimbaji dhahabu na madini  mengine nchini.
Aidha, taarifa hiyo ilidai kuwa Profesa Muhongo amelalamikiwa kwamba amepandisha gharama za ushuru wa uchimbaji wa madini kutoka Dola za Marekani 100 hadi 10,000.
Katika kukanusha, Wizara hiyo imefafanua; “Hakuna mwekezaji yeyote aliyezuiwa kuwekeza kwenye utafutaji na uchimbaji wa gesi nchini. Ikumbukwe kuwa vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi huwa vinatolewa kwa zabuni za wazi na za kimataifa na wala hazibagui kampuni wala utaifa. Zabuni hizi hutangazwa katika magazeti mbalimbali, tovuti  za  Wizara, Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) na   Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA).
Taarifa ya Wizara ambayo imechapishwa kwa kirefu katika gazeti hili, inaendelea kueleza kwamba wakati wa uombaji wa leseni,  mwombaji alitakiwa kulipa kiasi cha Dola za Marekani 50,000 kama ada ya maombi katika akaunti  ya TPDC ambazo hazirejeshwi hata kama mwombaji hajapata kitalu. Pia mwombaji alitakiwa kununua  data za kitalu alichohitaji kwa ajili ya kufanyia tathmini  na kuwasilisha tahmini hiyo kama sehemu  ya zabuni. Kwa upande wa baharini mwombaji alitakiwa kununua bid round data package kwa Dola za Marekani 750,000. Aidha mwombaji alitakiwa kununua 2D SPAN data package   kwa Dola za Marekani 3, 375,000. source raia mwema, may 5 2015

No comments

Post a Comment