Sunday, 17 May 2015

ALIYE KUWA MWANAFUNZI WA UDOM AKAMATWA KWA WIZI WA ZAIDI YA LAPTOP 40 PAMOJA NA SIMU ZAIDI YA 80 ALIZO IBA CHUONI HAPO

  Kamanda wa Polisi Dodoma DAVID MISIME - SACP akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) baada ya  kuwakamata ... thumbnail 1 summary


 

Kamanda wa Polisi Dodoma DAVID MISIME - SACP akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) baada ya  kuwakamata wezi watatu kutokana na wizi waliokuwa wakiendelea kuufanya mkoani Dodoma.
Baadhi ya laptop zilizoibiwa kwenye sehemu mbalimbali mkoani Dodoma zikioneshwa kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) mara baada ya kukamatwa wezi hao.
 Hivi ni vifaa vya kuvunjia vilivyokamatwa na jeshi la Polisi mkoa wa Dodoma
  Baadhi ya mabegi yaliyokuwa yametunza laptop pamoja na vifaa vilivyokuwa vinatumika kuibia


Na: Sylvester Onesmo wa Jeshi la Polisi Dodoma
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linamshikilia mtu mmoja aliyekamatwa katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Yarabi Salama (Yarabi Salama guest house) katika Manispaa ya Dodoma. Aliyekamatwa anafahamika kwa jina la MASAGARA S/O MESO, Mwenye miaka 40, Kabila Mzanaki wa Butihama, akiwa na funguo bandia 19, Master key 2, Bisibisi 2, Kisu kimoja, Tupa moja, Mikasi mitatu mikubwa ya kukatia vyuma, Msumeno ya kukatia vyuma mitano, Mitalimbo ya kuvunjia miwili, Adjustable spanner 1, Kipande cha bomba, Biti za kutobolea vyuma na mbao 8, Simu mbili aina ya Tecno na Nokia, Simu ya bandia ya Nokia, Pochi za mfukoni mbili, Hati ya dharura ya kusafiria, Betri ya simu moja, Nyenzo moja ya mbao, Nguo za kubadilisha, Madawa mbalimbali ya kienyeji, Kipande cha nondo kimoja na Irizi moja aliyokuwa amefunga sehemu ya juu ya mkono wa kushoto akiwa amehifadhi kwenye begi lake kwa maandalizi ya kufungua vyumba vya wapangaji wengine na kuvunja mita ili aibe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi DAVID MISIME – SACP amesema baada ya mahojiano na mtuhumiwa huyo, amekiri kufanya uhalifu wa kuvunja nyumba mbalimbali za kulala wageni na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu huko Mikoa ya Mwanza, Geita, Shinyanga, Tabora na hapa Dodoma. Uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini watuhumiwa wengine anaoshirikiana nao pamoja na matukio aliyofanya.

Kamanda MISIME amesema nimuhimu kwa wenye nyumba za kulala wageni kuwa makini na wageni wanaowapokea kwani baadhi yao wanapanga vyumba kwa lengo la kufanya uhalifu wa kuwaibia wateja wengine au vifaa vya hoteli kama TV, DVD Player, Ving’amuzi n.k na wakati mwengine hufanya vitendo vya wizi mitaani.

Pia Kamanda MISIME amesema katika hatua nyingine Jeshi hilo linamshikilia ONESMO S/O LUPILI YEYO Mwenye miaka 22, Muha, Mwenyeji wa Mkoa wa mwanza ambaye alikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu Dodoma (UDOM) Kitivo cha Sayansi ya Jamii mwenye namba za usajli T/UDOM/2013/01760 kozi ya Uhasibu mwaka wa kwanza ambaye alisimamishwa masomo baada ya kukosa sifa ya kuendelea na masomo chuoni hapo. Baada ya wanafunzi kulalamika mara kwa mara kuibiwa mali zao ndipo tulipofanikiwa kumkamata.

Mtuhumiwa huyo baada ya kuhojiwa alikiri kufanya uhalifu wa uvunjaji na wizi wa laptop na simu, alieleza kuwa mpaka anakamatwa na kuhojiwa alikuwa ameshaiba laptop zaidi ya 40 pamoja na simu zaidi ya 80 chuoni hapo.

Kamanda MISIME ameendelea kusema kuwa baada ya ufuatiliaji katika kumbukumbu za Polisi, jumla ya matukio 30 yameripotiwa katika kituo cha Polisi UDOM na jumla ya Laptop zinazokadiriwa kuwa zaidi ya 60 zimeibiwa katika vitivo mbalimbali ndani ya chuo hicho ikiwemo kitivo cha Sayansi ya Jamii na Elimu.

Mtuhumiwa huyo alipohojiwa zaidi alikwenda kuonyesha kwa mtu aliyemuuzia vitu hivyo baada ya kuiba, mtu huyo alibainika kuwa ni ISSACK S/O LEMA Mwenye miaka 29, Mkazi wa Airport ambaye ni fundi wa kutengeneza komputa maeneo ya Mtendeni Street Dodoma pembeni ya jingo la Bima.

Polisi walifika kwa mtu huyo na alipohojiwa alikiri kupokea Laptop zaidi ya 19 kutoka kwa mtuhumiwa ONESMO na imebainika fundi huyu mara baada ya kuletewa laptop na mtuhumiwa anazifungua na kuuza kifaa kimoja kimoja.

Kamanda MISIME ametoa wito kwa wanafunzi wa vyuo mbalimbli kuwa makini na baadhi ya wanafunzi waliosimamishwa na kufukuzwa chuo kwani imebainika ndio wanaoshikiana na wahalifu wengine kuiba vitu mbalimbali katika vyuo, pia wananchi nao wasinunue vitu bila ya kupewa risiti au kuandikishiana kwa mujibu wa sheria ili kujenga uaminifu kwa anayenunua na anayeuza mali la sivyo unaweza kushitakiwa kwa kukutwa au kupokea mali ya wizi. the choice may 17.2015

No comments

Post a Comment