Utafiti uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) umeonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2012/2013 watoto wa kike 228 walikatisha masomo kutokana na mimba za utotoni huku 42 wakilazimishwa waolewa
Ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana husababisha mimba katika umri mdogo.
Hii inatokana na ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi unatokana na imani potofu miongoni mwa jamii kwamba, kuwapatia elimu hiyo vijana ni sawa na kumruhusu kujihusisha na vitendo vya ngono.
Kutokana na imani hiyo, mimba katika umri mdogo zimekuwa zikiongezeka kwa kasi hivyo kukwamisha maendeleo ya wasichana walio wengi kwa kushindwa kutimiza malengo yao na kuishia kulea watoto bila kuwa na ajira.
Shule katika Wilaya ya Temeke ni miongoni mwa zile zinazokabiliwa na tatizo hilo kutokana na sababu mbalimbali.
“Mahali shule hizo zilipo ni kichocheo tosha cha wanafunzi kupata vishawishi vya kuingia katika mahusiano yasiyokuwa rasmi,” anasema Mkuu wa wilaya ya Temeke, Sophia Mjema.
Anasema wanafunzi hao hupata vishawishi kutoka kwa madereva wa magari ya mizigo yaendayo nje ya nchi kama vile Zimbabwe, Zambia na Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC).
Kutokana na hali hiyo, Mjema alisema ni lazima kila mwanafunzi ajitambue na kuzingatia kile kilichompeleka shule na kuzishinda changamoto anazokutana nazo.
“Kwa kufanya hivyo, vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa, wataweza kuepuka vishawishi na hivyo kuwa kichocheo cha maendeleo ya Taifa.
Kufanya vinginevyo, kwa mujibu wa Mjema, watakuwa wanajitengenezea mazingira yasiyo rafiki kwa maendeleo ya kiuchumi kwani itawalazimu kukatisha masomo yao na hivyo kutumia muda mwingi kulea mimba na baadaye mtoto.
“Katika ulimwengu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia, itakuwa ngumu sana kwa watu wasiokuwa na elimu ya kutosha kuendana na mabadiliko hayo,” Mjema anasema.
Anasema ni lazima vijana waandaliwa kwa kufahamu ipasavyo somo la afya ya uzazi vinginevyo atajiingiza katika mazingira yanayoweza kusababisha achanganyikiwe na kujikuta akiokota makopo ili aweze kupata chakula.
Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (Wama), chini ya Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete, wameanzisha kampeni ya kutokomeza mimba za utotoni tangu mwaka 2010.
No comments
Post a Comment