Kizza Besigye, kiongozi wa zamani wa chama cha upinzani cha FDC ametiwa mbaroni na vikosi vya usalama vya Uganda kwa tuhuma za kutaka kuitisha kikao kinyume cha sheria. Polisi ya Uganda imetangaza kuwa, Besigye ambaye ni mmoja wa wapinzani wakubwa wa serikali ya Rais Yoweri Museveni ametiwa mbaroni baada ya kuitisha mkutano kinyume cha sheria, mkutano ambao ulikuwa na lengo la kutoa wito wa kususia uchaguzi ujao wa Uganda uliopangwa kufanyika mwaka ujao. Mmoja wa maafisa wa polisi mjini Kampala amesema kuwa, Besigye ametiwa mbaroni pamoja na Meya Jiji la Kampala aliyeondolewa madarakani Erias Lukwago wakati walipokuwa wakipanga mikakati ya kuitisha maandamano ya kususia uchaguzi ujao. Wapinzani wa Uganda wamedai kuwa, lengo la kutiwa mbaroni mpinzani huyo ni kutaka kutia woga na hofu katika nyoyo za wapinzani hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu hapo mwakani. Kizza Besigye ambaye ameshindwa mara mbili na Rais Museveni katika kinyang’anyiro cha uchaguzi amekuwa akitiwa mbaroni mara kwa mara na vikosi vya usalama vya Uganda na kisha baadaye kuachiliwa huru.
redio tehran swahili mei 15, 2015
No comments
Post a Comment