Monday, 18 May 2015

Kuendelea kwa hali ya wasiwasi nchini Burundi

     Kuendelea kwa ghasia nchini Burundi hata baada ya kushindwa kwa jaribio la mapinduzi nchini hum... thumbnail 1 summary
    
Kuendelea kwa ghasia nchini Burundi hata baada ya kushindwa kwa jaribio la mapinduzi nchini humo ni kengele ya hatari kwa nchi zote za Afrika Mashariki na Kati. Umoja wa Mataifa umetoa taarifa ukitangaza kuwa zaidi ya Warundi laki moja wamekuwa wakimbizi kutokana na machafuko yanayoendelea nchini humo hata kabla ya jaribio hilo la mapinduzi. Wakimbizi hao kimsingi wamekimbilia nchi za Rwanda, Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Inaonekana kuwa kuzimwa kwa jaribio hilo la mapinduzi na askari watiifu kwa Rais Pirre Nkurunziza hakujasaidia pakubwa katika kuzima maandamano na malalamiko ya wananchi wanaopinga kushiriki tena rais huyo katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika baadaye mwezi ujao, bali kumeanzisha duru mpya ya machafuko na mvutano nchini humo. Sambamba na kufanyika safari ya Rais Nkurunziza mjini Dar es Salamu siku ya Jumatano kwa ajili ya kushiriki katika kikao cha viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, majenerali kadhaa wa jeshi walitangaza kupitia redio binafsi kuwa, walikuwa wamemuuzulu rais huyo wadhifa wake wa kuongoza nchi na kuvunja serikali yake kwa sababu alikuwa amekiuka katiba ya nchi kwa kutaka kushiriki tena katika uchaguzi mkuu. Baad ya kukamatwa majenerali hao, Nkurunziza aliwashukuru askari waliozima jaribio hilo la mapinduzi kutokana na radiamali yao ya haraka katika kulizima. Licha ya kutiwa mbaroni waliohusika na jaribio hilo lakini bado maandamano na malalamiko ya wananchi yanaendelea kuongezeka nchini siku hadi siku. Kuwepo kwa polisi na askari jeshi katika maeneo tofauti ya mji mkuu Bujumbura hakujasaidia pakubwa katika kuzima malalamiko hayo. Wapinzani wanasema kuwa wataendelea na maandamano hadi pale takwa lao la kumtaka Nkurunziza asigombee urais katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 26 Juni, litakapotekelezwa. Rais huyo ambaye anahudumia sehemu ya mwisho ya kipindi chake cha pili cha urais ametangaza kugombea kipindi cha tatu, jambo ambalo linachukuliwa na wapinzani kuwa linakiuka wazi katiba ya Burundi. Wakati huohuo, wanaharakati wa masuala ya kiraia wa Burundi huku wakipinga jaribio la mapinduzi ya kijeshi nchini, wamesema kuwa kufurahishwa wananchi na jaribio hilo ni ushahidi tosha kuwa wanataka mabadiloko katika ngazi za uongozi wa nchi hiyo. Jaribio hilo pia lilizua radiamali katika ngazi za kimataifa na kieneo. Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao walikuwa wanakutana huko Dar es Salaam kujadili mgogoro wa Burundi wamelaani vikali jaribio hilo. Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia siku ya Ijumaa alitoa taarifa akilaani jaribio hilo na kuelezea wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa kutokea vitendo vya kulipiza kisasi nchini humo. Alisema umoja huo utafanya kila liwezekanalo kwa lengo la kusaidia kumaliza mgogoro wa nchi hiyo. Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia pia imetaka kutekelezwa sheria na kurejeshwa nchi hiyo katika hali yake ya kawaida, haraka iwezekanavyo.

No comments

Post a Comment