Friday, 8 May 2015

Ligi Kuu isiendeshwe kimazoea

LIGI Kuu ya Tanzania Bara inakamilika leo huku jambo kubwa ambalo wakuu wanaoendesha ligi hiyo wameshindwa kulipatia jibu sahihi ni kuitanga... thumbnail 1 summary
Kiunga wa Yanga, Kotinho akimtoka beki wa Polisi Moro katika mechi iliyokutanisha timu hizo mbili.LIGI Kuu ya Tanzania Bara inakamilika leo huku jambo kubwa ambalo wakuu wanaoendesha ligi hiyo wameshindwa kulipatia jibu sahihi ni kuitangaza ligi hiyo pamoja na mipango mbadala.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Tanzania bado hawana mbinu mpya za kuweza kuiendesha ligi hiyo kisasa na kilichobaki ni kuiendesha kimazoea tu kama ilivyokuwa hapo awali. Ninasema hivyo kutokana na hali ilivyokuwa inaenda msimu mzima wa ligi hiyo kuanzia ilipoanza Septemba 20, mwaka jana hadi inafikia tamati leo Mei 9, 2015.
Kuna baadhi ya michezo ilikuwa inakosa mashabiki kabisa huku wenyewe wakiwa na kisingizio eti kwa sababu michezo inaoneshwa kwenye runinga basi mashabiki wanashindwa kwenda uwanjani. Huo ni uongo maana tumeshuhudia kwenye nchi nyingi michezo ikirushwa kwenye runinga na mashabiki wanaenda uwanjani.
Niwakumbushe tu kuwa kuna tofauti kubwa ya kuangalia mpira kwenye runinga na kuangalia mpira ukiwa uwanjani kwa sababu ukiwa uwanjani unapata mambo mengi na ukiangalia kwenye runinga kuna mambo mengi unakosa kuyaona. Wale wazoefu na haya mambo wataungana nami kwenye hili.
Hapa tatizo ni mfumo na mbinu mpya kutoka kwa wakuu wa ligi hiyo na kama nilivyosema hapo juu wao wanaongoza ligi hiyo kimazoea, wamekosa mtazamo mpya na wa kisasa. Kuna michezo miwili iliyochezwa katikati ya wiki nilitazama online kwenye runinga ya timu mbili kubwa za Simba na Yanga iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambayo uwanja ulikuwa mweupe kabisa.
Mechi ya kwanza ilikuwa Yanga na Stand United ya Shinyanga na Simba walicheza na Mgambo JKT ya Tanga yaani michezo hii ilikuwa na mashabiki wachache mno ukiongeza na ule mchezowa Mgambo JKT dhidi ya Azam FC uliochezwa jijini Tanga. Ninaweza kusema hii michezo ilitia fora kabisa hasa kutokana na ukubwa wa timu zenyewe.
Hapa jibu ni jepesi tu. Katikati ya wiki utampeleka nani uwanjani akatazame mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara wakati yupo kwenye harakati zake za kusaka mkate wake wa kila siku na hilo ndio jibu sahihi.
Tena ukizingatia muda wenyewe wa mchezo ndio hatari kabisa maana michezo hiyo ilianza mida ya saa kumi jioni ambayo wengi wao wanatoka katikati ya jiji kuelekea makwao na ukiongeza na msongamano wa magari au foleni, ndio kikwazo kabisa cha kukosa mashabiki.
Siku za nyuma hapa hapa nilishasema au kushauri kuwa hebu TFF waache panguapangua ya ratiba waje na ratiba ya maana ya uhakika ili michezo karibu yote ya Ligi Kuu ichezwe mwishoni mwa juma ila wenzangu hawa hawakunisikia hadi leo hii ninavyoandika makala haya, tumeshuhudia mechi zikichezwe katikati ya wiki.
Jambo la pili jamani hivi kinashindikana nini michezo mingine ya Ligi Kuu kuchezwa nyakati za jioni kuanzia muda wa saa 12:30 hadi tatu usiku. Nadhani muda hiyo huwezi kukosa mashabiki hasa kwenye miji ya pwani ya Bahari ya Hindi ambao wao kutoka nyakati za jioni ni tamaduni yao.
Hebu fikiria mechi kama zinahusu timu kubwa za Yanga na Simba eti inakosa mashabiki, si tatizo hili jamani maana timu hizo ndio timu kongwe ambazo zinaungwa mkono na mashabiki wengi wa soka nchini.
Hapa kuna tatizo kwenye Kitengo cha Masomo cha TFF au Bodi ya Ligi Kuu ambao wameshindwa kabisa kuja na mbinu mpya za kuitangaza ligi hiyo kwa mbinu za kisasa na wasipofanya hivyo, wakaendelea kufanya kazi kimazoea, basi hali itaendelea kuwa mbaya zaidi.
Ombi langu kwenu ni kuona ligi hiyo inabadilika na kwenda kisasa kama zilivyo kwenye nchi zingine na niwakumbushe tu kuwa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, hapa nyumbani Tanzania ndio nchi pekee yenye mashabiki wengi wa soka wenye wazimu wa ligi ya nyumbani kwa sasa kuliko nchini zingine za jirani.
Hivyo kazi kwenu kuweza kubadili mfumu wa uendeshaji. habari leo, 9 mei 2015

No comments

Post a Comment