Wachezaji wa Bayern Munich wakishangilia.
0
Zurich, Uswisi
Tayari timu nne zilizotinga hatua ya nusu fainali
ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2014/15 zimeishajulikana na ratiba ya mechi za
hatua hiyo imeishapangwa.
Timu hizo nne ni Barcelona, Real Madrid, Bayern
Munich na Juventus. Kwa mujibu wa ratiba ya hatua ya nusu fainali,
Juventus itakipiga na Real Madrid kesho mjini Turin huku keshokutwa
Barcelona ikiikaribisha Bayern Munich. Ratiba hiyo inaonyesha mechi za
marudiano zitachezwa wiki ijayo Mei 12 na 13.
Timu zitakazofanya vizuri katika hatua ya nusu
fainali zitatinga fainali itakayochezwa tarehe 6 Juni 2015 kwenye Uwanja
wa Olympic mjini Berlin, Ujerumani.
Barcelona v Bayern Munich
Kocha Josep Guardiola wa Bayern Munich atakipeleka
kikosi chake mjini Barcelona kwa ajili ya kuikabili Barcelona katika
mechi ya kwanza ya nusu fainali ambayo inatarajiwa kuwa na ushindani
mkubwa.
Ikumbukwe kwamba, Guardiola aliwahi kuinoa Barcelona na hii itakuwa ni mara yake ya kwanza kukutana nayo akiwa kocha wa Bayern.
Alipokuwa Barcelona, kocha Guardiola aliiongoza
timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya 2009 na 2011. Kwa
ujumla alipokuwa Barcelona kwa miaka minne aliiwezesha klabu hiyo kutwaa
mataji 14 mbalimbali.
Pia Guardiola aliwahi kuwa mchezaji wa Barcelona
na alikuwapo katika kikosi cha timu hiyo kilichotwaa ubingwa wa kwanza
wa kombe la Ulaya mwaka 1992.
Kihistoria, Barcelona na Bayern zimekutana mara
nane katika mashindano ya Ulaya, ambapo mwaka 1996 Bayern ilishinda 4-3
katika matokeo ya jumla katika mechi ya nusu fainali, mwaka huo Bayern
ilitwaa ubingwa.
Mara ya mwisho Barcelona na Bayern kukutana
ilikuwa ni katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2012/13, ambapo
katika mechi ya kwanza Bayern ilishinda 3-0 ugenini na katika mechi ya
marudiano Bayern ilishinda 4-0.
Takwimu zinaonyesha kwamba Bayern ambayo imetwaa
ubingwa wa Ulaya mara 5, imeshinda mechi tatu kati ya nne ilizocheza
kwenye Uwanja wa Barcelona.
No comments
Post a Comment