Mito mitatu imevunja kingo zake kutokana mvua zinazoendelea kunyesha
Habari zilizopatikana jana zimeeleza, mito mitatu
ya Kikavu, Weruweru na Kikuletwa inayomwaga maji yake katika Bwawa la
Nyumba ya Mungu imevunja kingo zake na kuingia katika makazi ya watu.
Kutokana na mafuriko hayo, watu wapatao 400 na 600
hawana mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kujaa maji, vyakula
kusombwa huku nguzo za umeme ziking’olewa na njia ya reli kufunikwa.
Vijiji ambavyo sehemu kubwa ya nyumba za wakazi
wake zimezingirwa na maji ni Uwanja wa Ndege, Kati, Langasani Magharibi
na Mashariki, Makumbusho na Riverside.
Mbali na athari hizo, Barabara ya Msitu wa Tembo
inayounganisha mikoa ya Manyara na Kilimanjaro, imefungwa kwa muda
kutokana na kujaa maji na hivyo kutishia usalama wa watumiaji wake.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Novatus Makunga alisema
mafuriko hayo ni makubwa kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 30
iliyopita kwa vile eneo kubwa limezingirwa na maji.
Aliupongeza uongozi wa TPC pamoja na Serikali ya
eneo lililoathirika kwa kuchukua hatua za haraka kuwasaidia wananchi
waliokumbwa na mafuriko. “Hakuna mtu aliyetegemea janga hili kwa hiyo
tunawaomba wadau mbalimbali wajitokeze kutoa misaada ya kibinadamu na
sisi kamati yetu ya maafa itakutana kesho (leo) kufanya tathmini,”
alisema.
Ofisa Mtendaji wa TPC anayeshughulikia Utawala,
Jaffar Ally alisema aliyekuwa eneo lililoathiriwa na mafuriko hayo
alisema eneo lote la kiwanda pamoja na ofisi zilikuwa ndani ya maji
kuanzia juzi usiku.
“Hivi tunavyoongea maji yameanza kupungua lakini
hali ilikuwa mbaya. Ndiyo tumeanza kunasua magari yaliyonasa kwenye
maji,” alisema Ally.
Alisema maji yaliyozingira kiwanda pamoja na
vijiji vya jirani yametokana na mvua kubwa zilizonyesha mikoa ya Arusha,
Manyara na Kilimanjaro na kutiririka katika mito.
“Mvua zilinyesha kuanzia maeneo ya Mbuguni,
Namanga na Mlima Kilimanjaro, ndizo zikaleta maji kwa wingi kwenye mito
inayomwaga maji Nyumba ya Mungu mpaka kingo zikashindwa kuhimili.” Hii
ni mara ya pili ndani ya muda usiozidi wiki mbili kwa vijiji vya Wilaya
ya Moshi vilivyopo ukanda wa Tambarare kukumbwa na mafuriko baada ya
yale yaliyotokea Aprili 21 na 22.
source; mwananchi, mei 5 2015 jumnne
source; mwananchi, mei 5 2015 jumnne
No comments
Post a Comment