Tuesday, 5 May 2015

Mahakama yamuidhinisha Nkurunziza Burundi

Mahakama ya katiba ya Burundi imemuidhinisha rais Pierre Nkurunziza kugombea muhula wa tatu, katika uamuzi ambao unatarajiwa kuwakasiris... thumbnail 1 summary


Mahakama ya katiba ya Burundi imemuidhinisha rais Pierre Nkurunziza kugombea muhula wa tatu, katika uamuzi ambao unatarajiwa kuwakasirisha zaidi waandamanaji wanaopinga rais huyo kugombea tena.
Mahakama hiyo imethibitisha uamuzi huo kupitia taarifa iliyotolewa Jumanne, huku maelfu ya waandamanaji wakimimika katika mitaa ya mji mkuu Bujumbura, kusema kamwe hawatokubaliana na uamuzi huo wanaoutaja kuwa kinyume na sheria.
Mwenyekiti wa chama tawala cha CNDD-FDD, Pascal Nyabenda, aliliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kupitia ujumbe mfupi wa simu baada ya kuulizwa juu ya uamuzi wa mahakama, kuwa tayari mahakama hiyo imepitisha uamuzi wa kumuidhinisha rais Nkurunziza kugombea muhula wa tatu.
Uamuzi huo umekuja wakati makamu wa rais wa mahakama hiyo Jaji Sylvere Nimpagaritse, akiripotiwa kuikimbia nchi hapo jana, huku polisi nayo ikiwauwa waandamanaji watatu mjini Bujumbura, na kufanya idadi ya waliouawa katika muda wa wiki moja kufikia watu 13.
Rais Pierre Nkurunziza baada ya kupitishwa na baraza la wazee wa chama chake cha CNDD-FDD kugombea muhula wa tatu. Rais Pierre Nkurunziza baada ya kupitishwa na baraza la wazee wa chama chake cha CNDD-FDD kugombea muhula wa tatu.
Gazeti la serikali ya Rwanda la New Times, liliripoti Jumanne kuwa makamu huyo wa rais wa mahakama ya katiba ya Burundi alikimbilia nchini Rwanda siku ya Jumatatu.
Jaji Nimpagaritse aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP, kuwa maoni ya wengi kati ya majaji saba wa mahakama hiyo waliamini itakuwa kinyume na katiba kwa Nkurunziza kusimama tena, lakini walikabiliwa na shinikizo kubwa na hata vitisho vya kuuawa kuwalaazimisha wabadili msimamo wao.

No comments

Post a Comment