Marakani imezuia kupitishwa hati ya kimataifa juu ya kuziondoa silaha za
nyuklia duniani baada ya nchi hiyo na washirika wake kulikataa
pendekezo juu ya kuzipiga marufuku silaha za nyuklia katika Mashariki ya
Kati.
Mazungumzo juu ya silaha za nyuklia yaliyohudhuriwa na wajumbe kutoka
nchi zaidi ya 150 yamekuwa yanafanyika kwenye Umoja wa Mataifa kwa zaidi
ya mwezi mmoja. Wajumbe hao walikutana ili kuutathmini mkataba juu ya
kuzuia uenezaji wa silaha za nyuklia, NTP. Lengo la mkataba huo ni
kuzuia kuzieneza silaha hizo na tekinolojia ya kuziundia.
Hata hivyo mazungumzo juu ya kulipitisha azimio linaloufafanua mpango wa
kuutekeleza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, yaligonga mwamba baada
ya nchi za kiarabu kutaka mkutano uitishwe ili kulijadili suala la
kuifanya Mashariki ya Kati liwe eneo pasipo na silaha hizo.
Nchi za kiarabu zilitaka mkutano huo uitishwe mapema mwaka
ujao. Lakini Marekani na washirika wake wamelipinga pendekezo hilo.
Israel iliyohudhuria mazungumzo hayo kwenye Umoja wa Mataifa, ingawa
haijautia saini mkataba wa kuzuia uenezaji wa silaha za nyuklia
ililipinga pendekezo la nchi za kiarabu.
Inaaminika kwamba Israel ndiyo nchi pekee yenye silaha za nyuklia katika
Mashariki ya Kati lakini haijakiri kuwa na silaha hizo. Naibu Waziri wa
Marekani wa udhibiti wa silaha Rose Gottemoeller amesema pendekezo la
kuitisha mkutano linaenda kinyume na malengo ya muda mrefu ya nchi yake.
Gottemoeller amehoji kwamba pendekezo juu ya kupiga marufuku silaha za
nyuklia katika Mashariki ya Kati halina matumiani ya kukubaliwa na nchi
zote.
Marekani imesema Misri na nchi nyingine za kiarabu zinajaribu kuuteka nyara mchakato wa mazungumzo kwa kuiwekea Israel masharti.
Wajumbe watoa mwito kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon.
Wajumbe waliokutana kwenye Umoja wa Mataifa kuitathmini hatua
iliyofikiwa katika kuutekeleza mkataba juu ya kupiga marufuku silaha za
nyuklia walitoa mwito kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kuitisha
mkutano mapema mwaka ujao bila ya kujali iwapo Israel na jirani zake
wanakubaliana na ajenda ya mkutano. Kutokana na mkutano huo Israel
inaweza kulazimika kukiri kwamba inazo silaha za nyuklia.
Kutokana utaratibu wa kupitishwa azimio kwa ridhaa ya washiriki wote,
uamuzi wa Marekani kuikataa hati iliyokusudiwa kupitishwa, maana yake ni
kwamba msingi wote juu ya kuondoa silaha za nyuklia dunianina kuzuia
uenezaji wa silaha hizo, umetenguliwa kwa muda wa miaka mitano ijayo
baada ya wiki nne za majadiliano.
Marekani iliungwa mkono na Canada na Uingereza. Mkutano mwingine juu ya
kuutathmini mkataba wa kupiga marufuku silaha za nyuklia unatarajiwa
kufanyika mnamo mwaka wa 2020. DW
Saturday, 23 May 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments
Post a Comment