Friday, 8 May 2015

MSUVA AITWA TAIFA STARS

KINARA wa ufungaji Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na mshambuliaji hatari wa Mabingwa wapya wa ligi hiyo, Yanga, Simon Msuva ni miongoni m... thumbnail 1 summary
Mshambuliaji hatari wa Yanga, Simon Msuva. Kwa mara ya kwanza ameitwa katika kikosi cha timu ya Taifa.KINARA wa ufungaji Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na mshambuliaji hatari wa Mabingwa wapya wa ligi hiyo, Yanga, Simon Msuva ni miongoni mwa wachezaji 28 watakaoingia kambini Jumatatu kujiandaa na michuano ya Baraza la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (COSAFA) inayoanza Mei 17, mwaka huu nchini Afrika Kusini.
Msuva ambaye ameitwa kwa mara ya kwanza pamoja na chipukizi wa Simba Ibrahim Ajib, wamekuwa na kiwango kizuri msimu huu, huku wachezaji wawili wa kulipwa, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wakikosekana kutokana na kufuzu kwa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuzu hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wachezaji walioitwa ni timu zao katika mabano ni Deogratius Munishi (Yanga), Aishi Manula, Mwadini Ally, Shomari Kapombe (wote Azam FC), Kelvin Yondani, Nadir Haroub (wote Yanga), Abdi Banda (Simba), Oscar Joshua (Yanga), Aggrey Morris (Azam FC), Isihaka Hassan (Simba) na Salim Mbonde (Mtibwa Sugar).
Wengine ni Erasto Nyoni, Amri Kiemba na Salum Abubakar (wote Azam FC), Said Juma Makapu (Yanga), Frank Domayo (Azam FC), Hassan Dilunga (Yanga), Said Ndemla (Simba), Haruna Chanongo (Simba), Mwinyi Kazimoto (Al-Makhiya, Qatar), Simon Msuva, Salum Telela (wote Yanga), Ajib, Mrisho Ngassa (Yanga), John Bocco (Azam FC), Juma Luizio (Zesco United), Mwinyi Haji (KMKM) na Kelvin Friday (Azam FC).
Akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye Ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Uwanja wa Karume, Ilala, Dar es Salaam, Nooij alisema ni lazima wachezaji wote waliotajwa hata kama ni majeruhi, wafike kambini kwenye Hoteli ya Tansoma kwa ajili ya kufanyiwa vipimo.
“Tunatawaka wachezaji wote wafike siku hiyo, watafanyiwa vipimowale watakaobainika ni majeruhi watabaki na kwa ajili ya matibabu kisha watasubiri mechi nyingine za Afrika,” alisema kocha huyo raia wa Uholanzi.
Nooij alisema kati ya wachezaji hao 28, 20 tu ndio watachaguliwa kwenda Afrika Kusini na wanane watabaki Dar es Salaam, na kwamba ikitokea baadhi wakaumia, waliobaki ndio watasafirishwa kuziba pengo, lakini kama sivyo, basi watasubiri kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Afrika na ile ya Wachezaji wa Ndani (CHAN).
Alisema kwa vile ligi bado inaendelea iwapo ikimalizika kuna ambao wataongezwa baada ya kumalizika kwa msimu kwa ajili ya michuano hiyo mingine ya Afrika.
Naye Mratibu wa Taifa Stars, Martin Chacha alisema katika michuano hiyo ya Cosafa itakayochezwa katika Jimbo la Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo, Stars inatarajiwa kucheza Mei 18, dhidi ya Swaziland na siku inayofuata dhidi ya Madagascar na kisha Lesotho.
Alisema wachezaji hao wataondoka Jumatano saa moja usiku kwa ndege ya Fastjet. Chacha alisema timu ikirudi kwenye mashindano hayo, itajiandaa tena kwa michuano ya Afrika dhidi ya Misri na CHAN ambapo inatarajiwa kucheza mchezo wa kwanza dhidi ya Uganda mwezi ujao. HABARI LEO MEI 8-2015

No comments

Post a Comment