Thursday, 7 May 2015

MSUVA ATIMKA YANGA

WINGA wa Yanga SC, Simon Msuva ameondoka jana kwenda Afrika Kusini kufanya majaribio ya kujiunga na klabu ya soka ya Orl... thumbnail 1 summary

Simon Msuva
WINGA wa Yanga SC, Simon Msuva ameondoka jana kwenda Afrika Kusini kufanya majaribio ya kujiunga na klabu ya soka ya Orlando Pirates ya huko, akikaidi maelekezo ya viongozi wake ya kusubiri hapo baada ya ligi kumalizika.
Habari zilizopatikana Dar es Salaam jana, zilisema Msuva aliomba ruhusa kwa uongozi wa Yanga juzi wakamkatalia, lakini jana alipanda ndege kwenda Johannesburg.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Jerry Muro alisema kuwa Pirates walileta mwaliko wa majaribio kwa ajili ya Msuva, lakini wakamuambia asubiri kwanza kwani atakwenda baada ya kumalizika kwa ligi.
“Najua kuna hiyo safari, ila aliambiwa asubiri amalize ligi atakwenda, kama amekwenda bila ruhusa atakuwa amefanya makosa,” alisema Muro.
Msuva aliyeibukia kituo cha soka cha Azam FC, ameondoka akiwa tayari ameipa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, huku pia akiwa anaongoza kwa kupachika mabao 17 akifuatiwa na mchezaji mwenzake wa timu hiyo, Amissi Tambwe mwenye mabao 14.
Tambwe ndiye mfungaji bora wa ligi msimu uliopita ambapo alipachika mabao 19 akiwa mchezaji wa Simba. Tangu ajiunge na Yanga mwaka 2012 akitokea Moro United, Msuva ameifungia timu hiyo mabao 35 katika mechi 102 za mashindano yote.

No comments

Post a Comment