Siku tatu zilizopita Waziri wa Fedha, Saada Mkuya aliwasilisha mwelekeo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2015/16.
Miongoni mwa vipaumbele alivyovitaja ni huduma za jamii na nyongeza kwa wafanyakazi.
Katika bajeti ya mwaka huu Serikali imekusudia
kupunguza utegemezi wa wafadhili kwa kuongeza makusanyo ya kodi kutoka
vyanzo mbalimbali nchini.
Tayari watu wa kada mbalimbali wameupinga mwelekeo
huo wa Bajeti wenye vipaumbele vinne ambavyo ni Uchaguzi Mkuu, kuweka
msukumo kwenye miradi ya umeme vijijini na maji vijijini na kuimarisha
rasilimali watu.
Katika mapendekezo hayo Serikali imepanga kutumia
Sh22.4 trilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo
ikiwa ni ongezeko la asilimia 15 ya bajeti iliyopita ya mwaka 2014/15
iliyokuwa Sh19.8 trilioni.
Kati ya fedha hizo, matumizi ya kawaida ni Sh16.7
trilioni na matumizi ya maendeleo ni Sh5.7 trilioni, sawa na asilimia
25.9 ya bajeti yote. Mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh 14.8 trilioni
sawa na asilimia 57.8 ya bajeti yote. Serikali inalenga kukusanya mapato
ya kodi ya jumla ya Sh13.3 trilioni sawa na asilimia 90.1 ya mapato ya
ndani.
Wakati nasoma taarifa za Serikali zilizowasilishwa
na Mkuya nilikumbuka zaidi maelezo aliyoyatoa mwaka jana wakati
akiwasilisha mapendekezo ya Bajeti ya 2014/15.
Licha ya mbwembwe nyingi za Serikali lakini mpaka
sasa imetekeleza chini ya asilimia 80 ya bajeti iliyopo na wakati huo
huo ikiongeza fedha kutoka Sh19.8 trilioni za bajeti iliyopo sasa hadi
Sh22.4 trilioni.
Zimeongezwa Sh2.9 trilioni lakini ukitizama
taarifa iliyowasilishwa na Mkuya utabaini kuwa kulikuwa na asilimia 38
tu ya fedha za maendeleo zilizotolewa.
Maana yake ni kwamba wakati bajeti iliyopo
inaelekea ukingoni fedha za maendeleo zilizotolewa hazijafikia hata
asilimia 50, huku Serikali ikieleza kuwa mwaka 2015/16 fedha za
maendeleo ni Sh 5.7 trilioni.
Mwaka jana Mkuya alitueleza kuwa makadirio ya
matumizi ya maendeleo ni Sh7.7 trilioni sawa na asilimia 39 ya matumizi
yote ya Serikali. Sasa kama kiasi hicho cha fedha ambacho ni zaidi kwa
Sh2 trilioni kwa bajeti ya 2015/16 hakikupatikana, kitapatikana hiki cha
Sh5.7 trilioni?
Bajeti ya mwaka 2013/14 ilikuwa Sh18.2 trilioni na
tulielezwa hayahaya na mwaka 2014/15 ikaongezeka hadi Sh19.6 trilioni
nyimbo zikawa zilezile na juzi tumeshuhudia tena ikiongezeka hadi Sh22.4
mambo bado ni yaleyale.
No comments
Post a Comment