Monday, 4 May 2015

Raia wa Kenya anaswa akivunja ATM Arusha

By John Mhala, Arusha MTU mmoja aliyetambulika kwa jina la Annuary Ally, raia wa... thumbnail 1 summary

MTU mmoja aliyetambulika kwa jina la Annuary Ally, raia wa nchi jirani ya Kenya ametiwa mbaroni na polisi baada ya kukutwa akivunja mashine ya kutolea fedha (ATM) ya Benki ya Barclays, Tawi la Stendi Kuu ya mabasi jijini hapa.
Kwa mujibu wa Ofisa Mikopo wa benki hiyo, Regina Kitali mtuhumiwa huyo alifika katika benki hiyo saa 5:15 asubuhi jana na kuingia katika mashine ya ATM kwa lengo la kutoa fedha.
Lakini baada ya dakika chache walisikia mtikisiko usiokuwa wa kawaida katika mashine hiyo na kumlazimu mmoja wa wafanyakazi wenzake kutoka nje kwenda kuangilia ni kitu gani.
Alisema baada ya mfanyakazi huyo kuingia ndani ya chumba hicho alimkuta Ally akiwa anajaribu kung’oa mashine hiyo ili apachike mashine maalumu aliyokuwa nayo kwa lengo la kuchukua fedha zilizokuwa ndani ya ATM hiyo.
Alisema baada ya kuona hali hiyo alimuuliza Ally kuna tatizo gani na kutaka kujua kama anahitaji msaada, lakini mtuhumiwa huyo alimjibu kuwa anataka kutoa fedha na alipotakiwa kupewa msaada alijifanya mbabe kwa kutaka kumtoa nje mfanyakazi huyo wa benki.
“Kufuatia hali hiyo mwenzetu alitoka nje mara moja na kubonyeza kengele ya tahadhari kuomba msaada kutoka kampuni ya ulinzi inayolinda katika tawi hili huku wengine tukipiga simu kuomba msaada wa polisi,” alisema.
Kwa mujibu wa Regina wakati mtuhumiwa akiendelea kung’oa mashine hiyo polisi wa kikosi cha FFU walifika eneo hilo na ndipo mtuhumiwa alipotoka nje na kuwaponyoka polisi na kuanza kukimbia kwa lengo la kutoroka.
Alisema walianza kupiga kelele za kuomba msaada ambapo raia wema walijitokeza na kuanza kumkimbiza mtuhumiwa huyo kwa kushirikana na polisi na kufanikiwa kumkamata katika eneo la benki ya NBC tawi la Meru huku akiwa na vitambulisho vingi vya aina mbalimbali pamoja na mashine hiyo maalumu.
Baada ya mtuhumiwa huyo kutiwa mbaroni alipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi kwa mahojiano zaidi ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Mmoja wa wapiga debe wa stendi kuu ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema mtuhumiwa huyo alionekana kama abiria stendi tangu majira ya saa moja asubuhi akirandaranda karibu na ATM hiyo kama abiria aliyekuwa amekwama usafiri kutokana na mgomo wa mabasi ulionza tangu alfajiri.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas hakuweza kupatikana kuzungumzia tukio hilo kwani alikuwa nje ya ofisi kikazi na simu yake ya kiganjani ilikuwa inaita bila majibu.
mei 5 2015 monday ; source habari leo

No comments

Post a Comment