rais wa burundi nkurunziza |
Ofisa mmoja wa jeshi la nchi hiyo, Meja Jenerali
Godefroid Niyombare alitangaza kuwa Jeshi la Burundi ‘limemtimua’ Rais
Nkurunziza na kwamba limeunda Serikali ya mpito kuiongoza nchi hiyo.
Mara tu baada ya taarifa hizo kuzagaa, Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais Jakaya Kikwete alilaani mapinduzi
hayo na kuitaka nchi hiyo kuahirisha uchaguzi hadi amani ya nchi hiyo
itakapotengamaa.
Vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa jana
mchana vilitawaliwa na habari za kupinduliwa Rais Nkurunziza, lakini
Ikulu ya nchi hiyo ilisema huo ulikuwa “utani” na kwamba jaribio hilo
lilikuwa limegonga mwamba na Nkurunziza bado ni rais wa nchi hiyo.
Tangazo la mapinduzi
Akizungumza kwenye redio moja binafsi ya Bonesha
FM, Jenerali Niyombare alisema: “Rais amekiuka Katiba na amekiuka
mazungumzo ya amani ya Arusha.
“Kwa kuwa Rais Nkurunziza anajiamini na amepuuza
jumuiya za kimataifa zilizomshauri kuheshimu katiba na mkataba wa amani
wa Arusha, tumemuondoa katika wadhifa wake pamoja na serikali yake.
“Ni muhimu kwa ajili ya kulinda heshima ya nchi...
Rais Pierre Nkurunziza ameondolewa madarakani,” alisema Jenerali
Niyombare ambaye alitimuliwa kazi na rais huyo mapema Februari mwaka huu
akiwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Usalama, Burundi.
Alisema atafanya kazi kwa kushirikiana na taasisi za dini na wanasiasa.
Habari zilizopatikana baadaye jana jioni, zilisema
Jenerali Niyombare alitangaza kufungwa kwa mipaka ya nchi hiyo,
barabara na viwanja vya ndege na hakuna mtu aliyeruhusiwa kuingia.
Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, lilisema kuwa hata waandishi wa habari wa kimataifa hawakuruhusiwa kuingia nchini humo.
Hata hivyo, jana jioni shirika hilo lilisema
taarifa ambazo hazikuthibitishwa ni kuwa kiongozi huyo wa mapinduzi
alikuwa amekamatwa na polisi wakati akikimbilia Ubalozi wa Marekani.
MWANANCHI
MWANANCHI
No comments
Post a Comment