Dar es Salaam. Makada watano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao
ni miongoni mwa wanaotajwa kutaka kuwania nafasi ya urais, wamefanya
uamuzi mgumu wa kutangaza kutogombea tena ubunge kwenye majimbo yao.
Wabunge hao na majimbo yao kwenye mabano ni Waziri
wa Uchukuzi, Samuel Sitta (Urambo Mashariki), Waziri Mkuu Mizengo Pinda
(Katavi) na Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa (Monduli).
Wengine ambao wanatajwa kuutaka urais na tayari
wametangaza kutogombea tena ubunge ni Spika wa Bunge, Anna Makinda
(Njombe Kusini), na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Benard Membe (Mtama).
Wakati wabunge hao wakitangaza kuachana na kiti
hicho cha uwakilishi, wengine; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika,
Stephen Wasira (Bunda), Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba (Bumbuli) na Waziri wa Maliasili na Utalii,
Lazaro Nyalandu (Singida Kaskazini) wamesema watarudi tena kwenye ubunge
kama watashindwa urais.
Walivyotangaza kuacha ubunge
Mei 26 mwaka 2013, Sitta alikaririwa na vyombo vya
habari akisema anafikiria kustaafu ubunge, na tayari ameshawaambia
wapigakura wa Urambo Mashariki juu ya azima yake hiyo.
“Viongozi wenzangu msipende kung’ang’ania
madaraka. Nawaombeni mjifunze kusema yatosha…staafuni kama ninavyotaka
kufanya mimi,” alisema Sitta katika Kongamamo la Mawasiliano katika
Nyanja za Digitali la wanafunzi wa Idara ya Uhusiano na Masoko, Chuo
Kikuu cha St. Augustine (Saut), Mwanza.
Kwa upande wake, Membe alitoa kauli ya kustaafu
ubunge Januari Mosi 2013 kwenye sherehe za Mwaka Mpya nyumbani kwake.
Alisema, “Unajua nimekuwa mbunge wenu kwa kipindi cha tatu. Hivi leo
ninawaaga rasmi kuwa sitagombea tena nafsi hii ya ubunge.”
Lowassa, amekuwa Mbunge wa Monduli kwa zaidi miaka
20 na kutokana na azma yake ya kutaka kugombea urais,, makada kadhaa wa
CCM wameanza kupigana vikumbo kumrithi.
Baadhi ya makada wanaoanza safari ya kumrithi
Lowassa Monduli ni aliyewahi kuwa Katibu Uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha na
Diwani wa Monduli Mjini, Loata Sanare na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa
Arusha, Namelok Sokoine, ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani
marehemu Edward Moringe Sokoine.
Pinda ambaye tayari ameshatangaza nia ya kugombea
urais alieleza Agosti 17, 2010 kuwa hatagombea tena ubunge katika
Uchaguzi Mkuu ujao.
Pinda aliirudia kauli hiyo katika mkutano wa
hadhara jimboni kwake akisema muda wa kuwa mbunge umetosha na sasa
anatafuta kitu kingine cha kufanya.
No comments
Post a Comment