Monday, 4 May 2015

SIMBA AMTAFUNA AZAM

SIMBA jana ilizidi kusogelea nafasi ya pili ya Ligi Kuu Tanzania Bara ili kucheza mashindano ya kimataifa msimu ujao baada ya kuibuka na ... thumbnail 1 summary
Wachezaji wa timu ya Simba, Ramadhan Singano (wa pili kulia mbele), Ibrahimu Ajib (kushoto aliyepiga magoti) na Awadhi Juma (kulia) wakishangilia baada ya kufunga bao la pili dhidi ya timu ya Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam jana. Simba ilishinda mabao 2-1. (Picha na Yusuf Badi).
SIMBA jana ilizidi kusogelea nafasi ya pili ya Ligi Kuu Tanzania Bara ili kucheza mashindano ya kimataifa msimu ujao baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo wa Simba unaiwezesha timu hiyo kufikisha pointi 44, inaendelea kuwa nyuma ya Azam FC yenye pointi 45, lakini Wana lambalamba hao wamebaki na michezo miwili mkononi wakati wekundu wa Msimbazi wamebaki na mechi moja.
Hata hivyo, pamoja na ushindi huo Simba bado ina nafasi finyu ya kumaliza ya pili kwani ikishinda mchezo wa mwisho itafikisha pointi 47 huku ikiombea Azam ifungwe mechi zote.
Kwa mara ya mwisho Simba ilitwaa ubingwa wa Tanzania Bara katika msimu wa 2011/12 na tangu wakati huo haijawahi kutwaa ubingwa huo.
Azam FC inahitaji pointi tatu tu ili itemize pointi 48, ambazo haziwezi kufikiwa na Simba wala timu nyingine yoyote na hivyo kuifanya kumaliza ya pili nyuma ya Yanga iliyotwaa ubingwa mapema.
Katika mchezo huo, Simba ndio ilikuwa ya kwanza kufunga bao katika dakika ya 49 kupitia kwa Ibrahim Ajibu baada ya kupata pasi ya Ramadhani Singano `Messi’.
Azam FC nao walisawazisha katika dakika ya 62 mfungaji akiwa ni Mudathir Yahaya aliyeingia kipindi cha pili baada ya kupata pasi ya Kipre Tchetche.
Dakika ya 75 Singano anaifungia Simba bao la pili akipiga mpira kutoka nje ya 18 baada ya kipa wa Azam FC kutoka nje ya goli. Azam FC waliongeza nguvu baada ya kumtoa Kavumbagu na kumuingiza John Boko, lakini mabadiliko hayo hayakuisaidia timu hiyo kwani jahazi lake lilizama.
Mshambuliaji Mganda wa Simba Emmanuel Okwi nusura afunge bao katika dakika ya 68 baada ya kupiga shuti lililopanguliwa kifundi na kipa wa Azam FC Aishi Manula.
Kutoka Tanga kwenye uwanja wa Mkwakwani wenyeji Coastal Union walichanua na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Stand United. Matokeo hayo yameifanya Coastal Union kufikisha pointi 31 ikiwa katika nafasi ya sita katika msimamo wa ligi hiyo.
Huko kwenye uwanja wa Manungu Turiani, wenyeji Mtibwa Sugar walipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ruvu Shooting.
Mabao ya Mtibwa Sugar yalifungwa na Mzamiru Yassin katika dakika ya 55 na Ame Ally katika dakika ya 65. Ushindi huo unaifanya Mtibwa iliyopo katika nafasi ya saba kwenye msimamo kufikisha pointi 31.

No comments

Post a Comment