Saturday, 23 May 2015

Tanzania haiwezi kupokea wazimbizi zaidi wa Burundi


Serikali ya Tanzania imesema kambi ya wakimbizi kutoka Burundi sasa imejaa na haiwezi kupokea watu zaidi hadi pale itakapopanuliwa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani Tanzania Issac Nantanga, akizungumza katika kambi ya Nyarugusu karibu na mji wa Kasulu mkoani Kigoma, amesema kambi hiyo ilivyo sasa haiwezi tena kupokea wakimbizi.
Ameongeza kuwa kambi mpya ya Nyarugusu II imeanza kujengwa na itakuwa karibu na kambi ya sasa. Amebainisha kuwa kambi asili ya Nyarugusu ilijengwa mwaka 1997 kwa ajili ya wakimbizi 50,000 waliokuwa wametoka nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kwamba kambi hiyo sasa ina wakimbizi laki moja. Tokea machafuko yaanze nchini Burundi wiki kadhaa zilizopota, Warundi 27,000 wamekimbilia Rwanda na wengine 9,400 wameingia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Tanzania imechukua wakimbizi zaidi ya 64,000 na hivyo kubeba mzigo mkubwa zaidi wa wakimbizi.
Machafuko yalianza Burundi Aprili 26 baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza uamuzi wake wa kugombea urais kwa muhula wa tatu mfululizo. Jana watu watatu walipoteza maisha kufuatia shambulizi la guruneti jijini Bujumbura. Polisi ya Burundi imesema  hujuma hiyo imetekelezwa na watu wasiojulikana waliovurumisha maguruneti mawili katika duka moja.

No comments

Post a Comment