Historia yake
Edward Lowassa alizaliwa Agosti 26, 1953 katika Kijiji cha Ngarash, Monduli na ndiye mtoto mkubwa wa kiume kwa Mzee Ngoyai Lowassa (atafikisha miaka 62 Agosti mwaka huu). Alianza kusoma katika Shule ya Msingi Monduli kati ya mwaka 1961–1967.
Kisha akaendelea kwenye Shule ya Sekondari Arusha kwa kidato cha kwanza mpaka cha nne kati ya mwaka 1968 - 1971, kabla ya kumalizia kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Milambo mkoani Tabora mwaka 1972–1973.
Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1974–1977 na kuhitimu Shahada ya Sanaa katika Elimu (B.A Education) na baadaye Chuo Kikuu cha Bath Uingereza kwa Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Maendeleo (mwaka 1983–1984).
Baada ya kumaliza chuo kikuu, Lowassa alifanya kazi ndani ya CCM akiwa ofisa wa ngazi ya juu kuanzia wilaya, mkoa na baadaye makao makuu kati ya mwaka 1977–1989.
Aliajiriwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC), mwaka 1989–1990.
Lowassa amemuoa Regina na wana watoto watano, wasichana wawili na wavulana watatu. Watoto hao ni Fredrick, Pamella, Adda, Robert na Richard.
Mbio za ubunge
Lowassa alichaguliwa kuwa Mbunge wa Monduli mwaka 1990 na 1993 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais (Haki na Mambo ya Bunge), kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Ardhi na Makazi akiwa Waziri mwaka 1993–1995.
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi (mwaka 1995), Lowassa alishinda ubunge kwa asilimia 87.3. Alikaa bila uteuzi wowote kwa miaka miwili. Mwaka 1997–2000, Rais Benjamin Mkapa alimteua kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Kuondoa Umasikini).
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 aligombea tena ubunge wa Monduli na kushinda kwa mara ya tatu. Rais Mkapa akamteua kuwa Waziri wa Maji na Mfugo hadi mwaka 2005.
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2005, aligombea ubunge na kushinda kwa asilimia 95.6. Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na Bunge likamthibitisha kwa kura 312.
No comments
Post a Comment