Monday, 11 May 2015

Hiki ndicho kinachovutia mbu kumuuma binadamu

Bara la Afrika hutumia Dola 12 bilioni za Marekani sawa na Sh22 trilioni  kila mwaka kwa ajili ya matibabu ya malaria. Ukitaja  mbu, wazo ... thumbnail 1 summary

Bara la Afrika hutumia Dola 12 bilioni za Marekani sawa na Sh22 trilioni  kila mwaka kwa ajili ya matibabu ya malaria.

Ukitaja  mbu, wazo litakalomjia mtu kwa haraka ni ugonjwa wa malaria. Hiyo inatokana na mazoea yenye ukweli kwamba, mdudu huyo hueneza ugonjwa huo kama ilivyo kwa malale na matende.

Lakini kuna baadhi ya mambo kuhusu tabia ya mbu ambayo watu wengi hawayafahamu, mbali  na sifa yake ya  kueneza magongwa, hasa malaria.

Hebu jiulize; hivi umewahi kukaa na wenzako watano lakini ukajikuta ni wewe peke yako ndiye unayelalamika kwamba unang’atwa na  mbu?

Kama umekutwa na hali hiyo,  basi unaweza kuwa mmoja wa watu walio kivutio kwa mbu.

Kwa kawaida, mvuto hutokana na harufu ya asili inayotoka mwilini mwa mtu anayeshambuliwa zaidi na mbu.

Wanasayansi wanasema kwamba mtu mmoja kati ya watano huwa kivutio cha mbu na kwamba mdudu huyo akinusa harufu ya mtu huyo, hata akiwa na wenzake zaidi wanne, basi atakwenda kwake na kwamba hata akifukuzwa, mbu huyo atarudi na kumuuma tena mtu huyo.

Daktari bingwa wa upasuaji wa Marekani, Joseph Mercola anasema kuwa kuna aina nyingi za mbu, lakini asilimia kubwa ya mbu wenye tabia hiyo ni mbu jike aina ya Anofelesi, ambao pia huambukiza malaria.

Anasema kuwa mbali na tabia hiyo mbu hao huvutiwa na maeneo yenye kemikali kwa kunusa harufu hiyo umbali wa mita 50 kutoka  walipo kabla ya kwenda kwenye eneo hilo. Mbu jike ndiyo huvutiwa zaidi na kupenda kunyonya damu ya binadamu kuliko mbu dume.

Dk Mercola ambaye ameandika majarida mbalimbali ya afya, anasema kuwa mbu jike hupendelea kufanya hivyo kwa sababu madini ya chuma na protini wanayonyonya kwenye damu ya binadamu huwasaidia kutengeneza mayai na baadaye kuzaliana.

Kutokana na hilo, wanasayansi wamebaini kuwa mbu huvutiwa na  bakteria.

Wanasema binadamu ana bakteria trilioni moja kwenye ngozi, lakini kati ya hao, asilimia 10 tu ndiyo hufanana kwa binadamu wote na asilimia nyingine hutofautiana, hali ambayo huchangia baadhi ya watu kuumwa zaidi na mbu kuliko wengine.
MWANANCHI

No comments

Post a Comment