- Alisoma katika shule za msingi Bunge na Isika zote za Arusha kati ya mwaka 1964–1972 na akajiunga na shule sekondari ya Wavulana Tabora alikohitimu kidato cha nne.
Historia yake
Makongoro Nyerere ni mtoto wa tatu wa Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kwa sasa ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala).
Makongoro alizaliwa Januari 30, 1956 (Amefikisha miaka 59 Januari mwaka huu).
Alisoma katika shule za msingi Bunge na Isika zote za Arusha kati ya mwaka 1964–1972 na akajiunga na shule sekondari ya Wavulana Tabora alikohitimu kidato cha nne.
Mwaka 1979 alijiunga na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na alipelekwa mstari wa mbele kwenye vita ya Uganda, kikosi cha Mizinga na baada ya vita yeye ni mmoja wa askari waliobakizwa ili kulinda amani ya wananchi wa Uganda lakini pia kufundisha askari wapya raia wa Uganda kwa ajili ya mipango ya baadaye ya kuilinda nchi yao wao wenyewe.
Aliporejea nchini kutoka vitani Uganda aliendelea kutumia jeshi kwa muda mfupi kabla ya kupelekwa katika Chuo cha Mafunzo ya Maofisa wa Jeshi (TMA), Monduli–Arusha na alishiriki na kufuzu mafunzo ya Ofisa Kadeti na akawa Ofisa wa Jeshi la Tanzania rasmi hadi alipostaafu rasmi mwaka 1990 akiwa na nyota mbili “Luteni”.
Baada ya kujiunga na kushiriki katika siasa kwa miaka mitano, aliamua kwenda nchini Scotland ambako alisoma Shahada ya Masuala ya Mikakati katika Chuo Kikuu cha Aberdeen, hii ilikuwa mwaka 2001 – 2003.
Makongoro ameshika nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM na wadhifa mkubwa aliowahi kushika ni uenyekiti wa chama hicho katika Mkoa wa Mara 2007–2012, lakini pia Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, moja ya vikao muhimu ndani ya chama hicho.
Makongoro amemuoa Jaji Aisha Nyerere na wamepata watoto watatu, wa kwanza anaitwa Julius Kambarage Nyerere, wa pili ni Daudi Nyerere na wa tatu ni Prince Nyerere.
Mbio za ubunge
Mwaka 1995, Makongoro Nyerere aliwashangaza Watanzania na hasa wanachama wa CCM baada ya kufanya uamuzi wa kukihama chama hicho na kujiunga na chama kilichokuwa maarufu sana wakati huo, NCCR Mageuzi.
Baada ya kujiunga NCCR, Makongoro alitangaza kuwa anagombea ubunge katika jimbo la Arusha Mjini kupitia NCCR. CCM ilifanya kila iwezalo lakini nguvu ya Makongoro ikawa kubwa, akapata asilimia 41.6 na kumshinda Felix Christopher Mrema wa CCM (Aliyewahi kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali) aliyenyakua asilimia 39.9, huku Mzee Edwin Mtei (Waziri Mstaafu wa Fedha na kiongozi wa Chadema wakati huo) akipata asilimia 13.5 ya kura zote. MWANANCHI MEI 8 2015
No comments
Post a Comment