Arusha. Katibu Mwenezi wa CCM mkoani Arusha, Isaack Joseph ametangaza kujitoa kwenye kinyang’anyiro cha kugombea ubunge katika Jimbo la Monduli mkoani Arusha.
Kada huyo wa CCM ambaye pia ni diwani wa Kata ya Monduli, alitangaza mwaka jana na mwaka huu mwanzoni kwamba angegombea ubunge katika Jimbo la Monduli kumrithi mbunge wa sasa, Edward Lowassa, ambaye anatajwa kutaka kuwania urais.
Hata hivyo, Joseph alisema hivi karibuni amelazimika kubadili nia yake hiyo kwa sababu mbalimbali, ikiwamo ushauri kutoka kwa wazee wa mila wa Kabila la Kimasai, maarufu kama Laigwanani.
Joseph alisema kuwa kwa mujibu wa mila na desturi za kabila hilo, wazee wa mila wana nafasi kubwa ya kushauri mambo mbalimbali kutokana na maono waliyonayo. Hivyo, baada ya kupokea ushauri huo, aliamua kusitisha mpango wake huo mara moja.
“Nimeshauriwa na wazee wa mila kwamba niondoe jina langu, wazee wameona hivyo na mimi siwezi kufanya kinyume na wao,” alisema Joseph ambaye alisisitiza kuwa badala yake sasa, ataendelea kujikita katika nafasi yake ya udiwani wa kata ya Monduli mjini. Hivi karibuni, baadhi ya wazee wa mila wilayani humo, walitangaza kumuunga mkono Namelok Sokoine baada ya kutangaza kumrithi Lowassa katika kiti cha ubunge, huku wakisema kuwa wanawake pia wana nafasi ya kuwania ubunge katika jimbo hilo.
Tamko la wazee hao lilikuja kufuatia kauli za baadhi ya watu wilayani humo kudai kwamba mwanamke hawezi kuwania nafasi ya uongozi wa juu kama ubunge na kuwaongoza wanaume kwa mujibu wa mila na desturi za Wamasai jambo linalopingwa na wazee hao wa mila.
Wachambuzi wa masuala ya siasa mkoani hapa, wameielezea hatua ya Joseph kuwa inatokana na kuhofia nguvu ya kisiasa aliyonayo Nemlok, ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani, marehemu Edward Sokoine.
Hata hivyo, mwenyewe amekanusha madai hayo akisema hayana msingi. “Nimejitoa kwa sababu ya ushauri wa wazee,” amesema.
Kujitoa kwa kiongozi huyo wa CCM kumeacha mbio za kumrithi Lowassa Monduli kubaki kwa wagombea watano; Daniel Porokwa, Namelock Sokoine, Julius Kalanga, Dk Salesh Toure na Japhet Sironga.
Hata hivyo, kwa kuwa muda wa kampeni bado, kuna uwekezekano wakatokea watu wengine.
No comments
Post a Comment