Mashirika ya kutetea haki za binadamu yametangaza kuwa, uchaguzi
wa kesho nchini Ethiopia hauwezi kuwa wa haki na kiadilifu kutokana na
ukandamizaji mkubwa uliofanyika nchini humo dhidi ya uhuru wa kutoa
maoni. Mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu yanaituhumu
serikali ya Ethiopia kwamba, inafanya ukandamizaji mkubwa dhidi ya
wapinzani, waungaji mkono wao na hata waandishi wa habari na kwamba,
serikali ya nchi hiyo imekuwa ikitumia kisingizio cha kupambana na
ugaidi kama wenzo wa kunyamazisha sauti za malalamiko na ukosoaji.
Ethiopia kesho inatarajiwa kufanya uchaguzi wa kwanza wa Bunge tangu
alipofariki dunia aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo Meles Zenawi.
Waziri Mkuu wa sasa Hailemariam Desalegn aliyemrithi Zenawi ana
matumaini ya kuendelea kubakia madarakani kupitia uchaguzi huo. Zaidi
ya Waethiopia milioni 36 na laki nane wamejiandikisha kupiga kura katika
uchaguzi huo. Uchaguzi wa kesho unahesabiwa na jamii ya kimataifa kama
mtihani muhimu wa kupima ahadi za serikali ya Addis Ababa za kukuza
demokrasia nchini humo. Chama tawala cha EPRDF kilichoko madarakani kwa
zaidi ya miongo miwili kina matumaini ya kushinda kikijivunia kile
kinachokitaja kuwa ni rekodi nzuri ya utendaji wa serikali hasa katika
uga wa uchumi.
Saturday, 23 May 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments
Post a Comment