Thursday, 14 May 2015

WABUNGE WA DAR WAJIPANGA KUMKWAMISHA MAGUFURI

MBUNGE wa Temeke, Abbas Mtemvu (CCM), amesema wabunge wa Dar es Salaam wanasubiri makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Ujenzi ili waikwamishe, k... thumbnail 1 summary
MBUNGE wa Temeke, Abbas Mtemvu (CCM), amesema wabunge wa Dar es Salaam wanasubiri makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Ujenzi ili waikwamishe, kutokana na kutotimiza ahadi ilizotoa kwa mkoa huo.

Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu
Zuberi Mtemvu

Akizungumza jana katika mjadala wa makadirio ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mtemvu alisema wabunge wote wa Dar es Salaam wanamsubiri Waziri wa Uchukuzi, Dk John Magufuli wamkwamishe kwa kuwa ahadi zake zimegeuka nyimbo.
Alisema Dk Magufuli alipokabidhiwa wizara hiyo, alisema amegundua dawa ya msongamano katika mji huo, lakini sasa anakaribia kumaliza muda wake msongamano huo umeongezeka, badala ya kupungua.
Alitoa mfano wa ahadi ya ujenzi wa barabara za Juu na kufafanua kuwa ahadi hiyo kila mara imekuwa wimbo kuhusu upembuzi yakinifu, huku msongamano ukizidi kuongezeka.
Mtemvu aliwaomba wabunge wote kwa kuwa sehemu kubwa wana makazi katika jiji hilo, kushirikiana na wabunge wa Dar es Salaam kupata kauli moja ya Bunge kuhusu msongamano kwa kuwa na wao wanaathirika.
Kwa mujibu wa Mtemvu, karibu kila mbunge akisimama anazungumzia jimbo lake, wakati ana makazi katika jiji hilo ambalo pamoja na kuchangia karibu asilimia 75 ya pato la Taifa, lakini linasumbuliwa na msongamano mkubwa wa magari.
Aliomba Serikali pia itenge posho na vifaa kwa askari wa Usalama Barabarani wa jiji hilo, ambao wamekuwa wakifanya kazi usiku na mchana na hasa wakati wa mvua.
Alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kufanya ziara kutembelea waathirika wa mafuriko, yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Mbunge wa Viti Maalumu, Zarina Madabida (CCM), aliitaka Serikali itenge fedha kwa ajili ya marekebisho ya barabara zilizoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha.
Alibainisha kuwa wabunge na madiwani wa Dar es Salaam, waliamua kujenga barabara za pete au za pembezoni hafifu za lami badala ya za changarawe, ili kuepuka kufanya marekebisho ya mara kwa mara.
Uamuzi huo kwa mujibu wa Madabida, ulisababisha msongamano wa magari kupungua kwa kuwa magari mengi yalitumia barabara hizo zilizokuwa zikipitika.
Hata hivyo, alisema kuwa mafuriko yaliyokumba jiji hilo yameharibu barabara hizo hafifu za lami na msongamano unaoonekana, umetokana na watu kurejea katika barabara kuu kwa kuogopa kuharibika kwa barabara hizo za pete.

No comments

Post a Comment