Friday, 8 May 2015

Wakenya wafuatilia uchaguzi Uingereza

    Wakenya wafwatilia uchaguzi Uingereza Uchaguzi wa bunge la 56 la Uingereza umekuwa ukifu... thumbnail 1 summary

   

Wakenya wafwatilia uchaguzi Uingereza
Uchaguzi wa bunge la 56 la Uingereza umekuwa ukifuatilia kwa makini nchini Kenya ambapo hafla maalum imeandaliwa katika makaazi ya ubalozi wa Uingereza katika mji mkuu Nairobi.
Raia wa Uingereza wanaoishi Kenya, walijumuika na Wakenya na wanadiplomasia katika hafla hiyo mapema leo.
Walikusanyika kusubiri matokeo ya uchaguzi huku wakifuatilia matokeo kupitia televisheni zilizotundikwa kwenye bustani .
Umuhimu ilikuwa sio tu kutaka kujua mshindi katika uchaguzi huu bali pia, maslahi tofauti kwa jamii nchini Kenya kutokana na misimamo na sera tofauti za vyama vilivyogombea katika uchaguzi huu.
Hii ni pamoja na sera za nchi za nje, masuala ya kiuchumi na biashara, masuala ya uhamiaji na msimamo wa Uingereza kuhusu kusalia au kujitenga na Umoja wa Ulaya, yote haya yakiwa ni miongoni mwa ahadi walizotoa wagombea kwa wapiga kura wakati wa kampeni zao.
Miongoni mwa waliokuwepo ni aliyekuwa waziri mkuu nchini Kenya Raila Odinga, ambaye ameeleza kuridhishwa kwake na namna Uingereza imefanikiwa kuanda uchaguzi huu.
Wakenya wafwatilia uchaguzi Uingereza
Amesema ni mfano mzuri kwa nchi za Kiafrika kuiga.
''Huo ni mfano mzuri ambao mataifa ya Kiafrika hayana budi kuiga kwani tofauti na Uingereza, ghasia zimekuwa zikishuhudiwa katika baadhi ya mataifa ya Afrika ''
''Viongozi wengi wa Afrika hawakubali matokeo ya uchaguzi '' Alisema Bw Odinga.
Na sio tu wanasiasa, mabalozi,na wasomi walioona umuhimu wa kufuatilia matokeo ya uchaguzi huu wA Uingereza, bali pia kulikuwemo msanii wa mtindo wa Hip Hop kutoka Kenya Octopizzo.
Kiongozi wa upinzani Kenya Raila Odinga akizungumza na BBC
''Nimefurahishwa sana jinsi uchaguzi huu ulivyopangwa na haswa nidhamu ya vyombo vya habari vya Uingereza''.
''Hawakutangaza chochote kuhusu wagombea na kampeni punde tu baada ya kumalizika kwa muda maalum wa kampeni na kuanza kwa uchaguzi huo''.Alisema Henry Ohanga al-maarufu OctoPizzo.
''Hilo linasaidia kuondosha ushawishi wa vyombo vya habari kwa wapiga kura'' aliongozea Octopizzo.
Wengi wanafuatilia uchaguzi huo kutokana na uhusiano wa Kenya na Uingereza .
Uingereza ni mojawapo ya nchi zenye ushawishi mwingi duniani na hivyo, sera zitakazoidhinishwa zitakuwa na ushawishi katika sehemu nyingine duniani, likiwemo bara la Afrika kwa kutegemea nani au chama kipi kitakachoingia madarakani. bbc mei 8, 2015

No comments

Post a Comment