ZAIDI ya walimu 1,200 wanatarajiwa kukutana na Rais Jakaya Kikwete
mjini Arusha, wiki ijayo wakati kiongozi huyo wa nchi atakapokuwa
akifungua rasmi mkutano wao mkuu wa mwaka kitaifa.
“Tunatarajia kuwa walimu wapatao 1,200 kutoka mikoa 25 na wilaya 153 za Tanzania Bara watakutana na Rais Kikwete katika eneo la Ngurdoto, wilayani Meru, mkoani Arusha.
Mkutano huo Mkuu wa Chama cha Walimu Taifa (CWT) utafanyika kati ya Mei 26 hadi 28, mwaka huu,” alisema Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Arusha, Juvin Buruya na kuongeza: “Walimu wote Tanzania watawakilishwa vema kwenye mkutano huo ambapo tutatumia fursa ya uwepo wa Rais Kikwete kumuomba amalizie ahadi zake kadhaa alizowaahidi wakufunzi hao kabla hajastaafu rasmi,” alisema.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo wa CWT mkoani Arusha, walimu watakaojumuika kwenye mkutano mkuu, watatumia fursa hiyo kumuaga rasmi mke wa Rais, Mama Salma Kikwete ambaye pia ni mwalimu.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CWT, Ezekiah Oluoch alisema chama hicho kimekuwa kikipata ushirikiano mzuri kutoka serikali ya awamu ya nne, na kwamba wanatarajia uhusiano huo mzuri kuendelea hata katika serikali ijayo ya awamu ya tano.
No comments
Post a Comment