NAIBU
Waziri wa Elimu, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa, Kassim Majaliwa amewataka walimu nchini kujiepusha na mambo
yanayochangia kukiuka misingi ya haki za binadamu na maadili mema.
“Mwalimu ni kioo cha jamii kuweni raia wema, chukieni maovu na kuweni mfano bora kwa jamii kwa kauli na matendo ili jamii ijifunze kutoka kwenu,” alisema Majaliwa.
Alisema hayo jana mjini hapa wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya haki za binadamu kwa walimu wa shule za sekondari, wakaguzi wa shule na wakufunzi wa vyuo vya ualimu kutoka mikoa ya Dodoma, Singida na Manyara.
Mafunzo hayo yamedhaminiwa na Shirika la Mipango ya Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). Alisema ni jambo jema kama walimu watakuwa mfano wa kuigwa katika jamii na kuwa mabalozi wema na watetezi wa haki za binadamu, hususan watoto na watu wenye ulemavu kwa imani na vitendo na hatimaye kuongeza tija kazini.
“Baadhi ya walimu wamekuwa wakifanya kazi bila kuzingatia maadili ya kazi zao, kuendekeza rushwa, kutoa huduma zisizokidhi matarajio ya wananchi na hivyo kusababisha malalamiko ya wananchi dhidi ya serikali,” alisema.
Alisema ipo haja kubwa ya kueneza elimu ya haki za binadamu katika jamii ili haki hizo ambazo zimeainishwa katika katika ya nchi, sheria mbalimbali na mikataba ya haki za binadamu.
Naibu Waziri alisema katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na matukio mengi ya ya uvunjifu wa haki za binadamu ikiwemo ukatili dhidi ya watoto, vurugu na migomo katika shule na vyuo na matukio mbalimbali ya uhalifu yakiwemo wananchi kujichukulia sheria mkononi dhidi ya watuhumiwa wa uhalifu.
Alisema matukio mengine ni ukatili dhidi ya wanawake mauaji ya walemavu wa ngozi na vikongwe na ajali za barabarani matukio ambayo yanaashiria kuna uelewa mdogo dhidi ya haki za binadamu.
Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na utawala bora, Dk Kelvin Mandopi alisema tume hiyo iko katika utekelezaji wa mpango kazi wa kitaifa wa haki za binadamu wa mwaka 2013 hadi 2017 kwa lengo la kukuza na kulinda haki za binadamu nchini.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa UNDP, Godfyey Mbisa alisema lengo la programu hiyo ni kurahisisha ufundishaji wa haki za binadamu na kuzipa uzito unaostahili.
No comments
Post a Comment