Rombo. Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Lembris Kipuyo
amesema tatizo la ulevi kupindukia wilayani humo, limewaathiri wanaume
kiafya na kuwataka watendaji kulivalia njuga.
Kutokana na ulevi huo, kuna madai kuwa baadhi ya
wanawake wanaoishi kwenye ndoa wilayani huo, wamelazimika kutafuta
wanaume nchi jirani ya Kenya ili wapate mimba kutokana na waume wao
kuzidiwa na ulevi, hivyo kushindwa kuwahudumia.
Kipuyo alisema tatizo la ulevi wilayani humo limefikia hatua ya hatari zaidi na jitihada za haraka zinahitajika.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha baraza
la madiwani la halmashauri hiyo, Kipuyo alilitaja eneo lililozidiwa na
ulevi kuwa ni Kikelelwa lililopo Tarakea, mpakani mwa Tanzania na Kenya.
“Tatizo la ulevi wilayani Rombo na matumizi ya
pombe zisizokuwa na viwango ni kubwa sana na linahitaji nguvu ya pamoja
kulikabili,” alisema na kuongeza:
“Imefikia mahali wanaume wengi wanashindwa kumudu
kufanya tendo la ndoa na kuwalazimu wanawake wao kukodi wanaume kutoka
nchi jirani ya Kenya kwa ajili ya tendo hilo.”
Alisema ni vizuri mamlaka husika, zikiwamo
Serikali za vijiji kuhakikisha ulevi unakwisha ili kuepuka Tarakea kuwa
kizazi cha Wakenya.
Alisema kuwa viongozi na watendaji wakisimamia vyema suala hilo, unywaji wa pombe hasa zile zisizokuwa na viwango litakwisha.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Anthony Tesha
alisema viongozi wameshindwa kukemea suala la ulevi na badala yake
wameliacha suala hilo kwenye ofisi yake.
Tesha alisema watendaji kwa kushirikiana na
madiwani wana uwezo wa kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha Rombo
inaondokana na ulevi.
No comments
Post a Comment