Dar es Salaam.Nahodha wa timu ya taifa ya
Tanzania ‘Taifa Stars’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na kiungo Amri Kiemba
wameachwa katika kikosi cha timu hiyo kinachotarajiwa kuondoka leo
jioni kwenda Afrika Kusini kushiriki mashindano ya Kombe la Cosafa.
Kocha wa timu hiyo Mart Nooij amewaacha wachezaji sita katika kikosi hicho kutokana na sababu mbalimbali.
Cannavaro ameachwa kutokana na kuwa majeruhi wa
kifundo cha mguu aliyoyapata katika mchezo wa kwanza wa Kombe la
Shirikisho dhidi ya Etoile du Sahel ya Tunisia uliofanyika jijini Dar
es Salaam.
Nahodha huyo anaungana na wachezaji wengine
majeruhi walioachwa ambao ni kipa Aishi Manula, beki Hassan Isihaka na
mawinga Haroun Chanongo na Kelvin Friday wakati Kiemba ameachwa
kutokana na matatizo ya kifamilia.
“Baada ya kupimwa afya na madaktari wamebaini
Manula, Isihaka, Chanongo, Friday na Cannavaro bado ni majeruhi na
hawatasafiri na timu kesho.”
“Watabaki nchini wakiendelea kufanya mazoezi chini
ya ungalizi mpaka timu itakaporejea kutoka Afrika Kusini na kuungana
kwa ajili ya maandalizi ya Afcon,” alisema Ofisa Habari wa TFF, Baraka
Kizuguto. Kuhusu Kiemba ambaye uteuzi wake ulizua gumzo kutokana na
kiungo huyo kukosa namba ya kudumu katika kikosi cha Azam kwa sasa,
Kizuguto alisema Kiemba amepewa ruhusa kutokana na kuwa na matatizo ya
kifamilia.
Kizuguto alisema msafara wa Taifa Stars utaongozwa
na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa TFF, Ephaphra Swai ukijumuisha
wachezaji 20 na benchi la ufundi na timu hiyo inatarajiwa kufikia katika
Hoteli ya Sun City iliyopo pembeni kidogo ya Jiji la Rusterburg.
Michuano ya Cosafa itaanza Mei 17 hadi Mei 30,
kwenye viwanja vya Olympia Park na Moruleng katika Jimbo la North West
Province nchini Afrika Kusini.
MWANANCHI
MWANANCHI
No comments
Post a Comment