Dodoma. Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu jana alichafua hali ya hewa bungeni baada ya kudai kuwa Serikali ya Awamu ya Nne ni ya kichovu, kauli ambayo ilizua mabishano makali kati yake na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama.
Akichangia Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu 2015/16,
Lissu alisema Serikali hiyo imeshindwa karibu kila jambo, ikiwamo
uandikishaji wa wananchi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Alisema uchovu huo pia umejidhihirisha wazi baada
ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kueleza kwamba mpaka sasa haijapewa
fedha za maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, wakati imebaki miezi
mitano ufanyike.
Lissu alivutana na Spika Anne Makinda pale
alipotakiwa kukaa chini kumpisha Mhagama azungumze baada ya kugoma kwa
maelezo kuwa waziri huyo ameingilia wakati akitoa ufafanuzi wa uchovu wa
Serikali.
Mvutano huo ulianza Lissu alipokuwa akisema kuwa
mbali na kukwama kwa uandikishaji katika Daftari la Wapigakura, hata
katika upigaji wa kura za kupitisha Katiba Inayopendekezwa katika Bunge
Maalumu la Katiba, marehemu, mahujaji na wagonjwa ni miongoni mwa
wajumbe wa Bunge hilo waliopiga kura.
“Hata Uchaguzi Mkuu mpaka sasa Serikali haijatoa
fedha kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, hakuna maandalizi yoyote.
Hatukubali kuona Serikali hii ikijiongezea muda kwa kisingizio hicho,”
alisema Lissu.
Kauli hiyo ilimwinua Mhagama na kueleza kuwa
katika Bunge la Katiba zilipigwa kura halali, huku akifafanua jinsi
Serikali ilivyofanya shughuli nyingi za maendeleo.
“Mheshimiwa Spika, Lissu analidanganya Bunge.
Kauli zake ni za kuudhi namwomba asiendee kupotosha umma,” alisema
Mhagama huku Lissu akisisitiza kauli yake.
Wakati Mhagama akisimama kuomba utaratibu wa
Spika, Lissu naye alisimama akipinga kitengo cha kukatizwa na waziri
huyo kuchangia, tukio ambalo liliingiliwa na Spika na kuzua majibizano.
“Huyu ananizuia kwa misingi gani, kafuata
utaratibu upi,” alisema Lissu huku Mgahama naye akiendelea kuzungumza
huu akiwa amesimama kabla ya wote wawili kukatishwa na Spika Makinda
aliyewataka wakae chini na kufafanua kuwa yeye ndiye anayejua utaratibu.
Baada ya kutoa ufafanuzi huo, Makinda alimpa
nafasi Mhagama kuendelea kuzungumza na alipomaliza alimpa nafasi Lissu
ili amalizie kuchangia hotuba hiyo.
MWANANCHI
MWANANCHI
No comments
Post a Comment