Tuesday, 19 May 2015

NATO: Tupo tayari kuisaidia kiulinzi serikali ya Libya

Shirika la Kujihami la Nchi za Magharibi NATO ... thumbnail 1 summary

Shirika la Kujihami la Nchi za Magharibi NATO limetangaza kuwa, lipo tayari kutoa msaada wa kiulinzi kwa serikali ya Libya. Hayo yamesemwa na Jens Stoltenberg, Katibu Mkuu wa shirika hilo kando ya kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi wa jumuiya hiyo huko mjini Brussels, Ubelgiji kikao ambacho kimeitishwa kwa lengo la kuchunguza njia za kukabiliana na magendo ya binaadamu. Stoltenberg amesema kuwa, sanjari na NATO kuunga mkono juhudi za Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kufikiwa makubaliano ya kisiasa na pande za mapigano nchini Libya, lakini pia iko tayari kuipatia nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika msaada wa kiulinzi ili iweze kuunda serikali ya umoja wa kitaifa. Aidha katibu mkuu huyo wa NATO amekaribisha mazungumzo ya kina baina ya Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kupambana na wimbi la uhamiaji haramu barani Ulaya. Suala la wahamiaji haramu kutumia maji ya Libya kuelekea barani humo na hatari inayotokana na magendo hiyo, limeitia wasi wasi jamii ya kimataifa. Ni vyema ifahamike hapa kwamba, mashambulizi ya kijeshi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi NATO dhidi ya Libya, hapo mwaka 2011, yamepelekea taifa hilo kutumbukia katika dimbwi la machafuko makubwa yanayotokana na ukosefu wa usalama nchini humo.

No comments

Post a Comment