Friday, 8 May 2015

NYANZA: Walimu wageuza madaftari viti

Geita . Walimu wa Shule ya Msingi Mwatulole mkoani Geita, hawana meza wala viti hali inayowalazimu kukalia madaftari ya wanafunzi kwa kuyat... thumbnail 1 summary
Geita. Walimu wa Shule ya Msingi Mwatulole mkoani Geita, hawana meza wala viti hali inayowalazimu kukalia madaftari ya wanafunzi kwa kuyatandika kwenye magogo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti juzi baada ya kukutwa wamekalia madaftari, walimu hao walisema ukosefu wa samani shuleni hapo unawaathiri katika ufundishaji.

“Wakati mwingine tunasahihisha madaftari, huku tumesimama,” alisema Mwalimu Mathias Matiginya na kuongeza:

“Unakuta mwalimu ana vipindi vinne kwa siku, lakini anaishia kufundisha viwili kutokana na kusimama muda mrefu, anachoka haraka.”

Pia, alisema shule hiyo ina walimu wengi na haina ofisi, viti wala meza, hivyo walimu wanatumia darasa kama ofisi.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Catherine Mgisu alisema suala hilo limefikishwa kwa uongozi wa halmashauri na kamati ya shule.

Alisema kamati hiyo inafanya jitihada za kuhamasisha wazazi kusaidia maendeleo ya shule ikiwamo upatikanaji wa viti na meza za walimu.

“Hii shule ina changamoto nyingi siyo ukosefu wa vitu hivyo tu, bali ina wanafunzi wengi, uhaba wa madarasa na madawati pamoja na utoro wa wanafunzi,” alisema Mwalimu Mgisu.

Katika hatua nyingine; Mwalimu wa Taaluma, Salma Rajab alisema anakerwa na wingi wa wanafunzi.

Alisema kutokana na hali hiyo  kipindi cha mitihani mbanano huwa mkubwa hali inayowanyima fursa ya kusimamia vizuri.

“Walimu tunapata shida hasa wanafunzi wanapofanya mitihani, tunashindwa kupata uhalisia wa matokeo yao. Huwa hatulitawali darasa kutokana na msongamano, hivyo tunakaa nje,” alisema Mwalimu Rajab. Mwalimu Debora Lucas alisema darasa moja linachukua zaidi ya wanafunzi 3,000.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita, Magarita Nakainga alisema alipokea taarifa ya changamoto hizo na kwamba suala hilo linashughulikiwa ili kuhakikisha shule inakuwa na hali nzuri.
mwanachi mei 8 2015

No comments

Post a Comment