Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete jana alionekana kukerwa waziwazi na kitendo cha polisi kuwazonga na kuwasukuma wananchi waliokusanyika eneo la Jangwani kumsikiliza.
Tukio hilo lilitokea alipotembelea maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Baada ya kufika eneo hilo saa tisa alasiri, polisi
waliokuwa wakiimarisha ulinzi walianza kuwasukuma wananchi hasa kule
walipokuwa wakielekea alikokuwa Rais Kikwete.
Mara kadhaa, Rais Kikwete alisikika akiwataka polisi kuacha kuwabugudhi badala yake wasogee upande wake.
Kutokana na askari hao kutotii amri yake,
alimwagiza Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman
Kova aliyekuwapo kuwakataza askari hao.
“Jamani, waacheni waje kwa nini mnawapiga? Mbona
hamsikii? Kova hebu waambie askari wako wawaache kuwasumbua,” alisikika
Rais Kikwete akisema huku akionyesha mkono kwa ishara ya kuwaita
wananchi wasogee upande wake.
Baada ya agizo hilo, Kamanda Kova aliwazuia askari kuwasukuma wananchi na ndipo walipoacha.
Akiwahutubia, Rais Kikwete alimwagiza Mhandisi wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Eliseus Mtenga kuchukua hatua za haraka
kushughulikia changamoto ya kuziba kwa Daraja la Jangwani ili kudhibiti
mafuriko yanayoendelea kuathiri wakazi wa eneo hilo.
Alisema hakuna sababu ya kuagiza Jeshi la Ulinzi
la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kushughulikia changamoto hiyo kwa kuwa
ni kazi ndogo inayoweza kutafutiwa ufumbuzi kwa muda mfupi.
“Huu uchafu ni wa kuondoa haraka, hakuna sababu ya
kuleta wanajeshi hapa. Mvua hizi bado zinanyesha, tusisubiri hali
iendelee kuwa mbaya,” alisema Rais Kikwete.
Mhandisi Mtenga aliahidi kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo haraka.
Katika hatua nyingine; mvua zinazoendelea kunyesha
zimesababisha Shule ya Msingi Msasani kujaa maji, kuvunjika madaraja na
kupanda kwa gharama za bidhaa ikiwamo chakula.
mwananchi.
mwananchi.
No comments
Post a Comment