MADAI ya wanawake wa wilaya ya Rombo, Kilimanjaro, kukodi wanaume
kutoka nchini Kenya, baada ya kukosa huduma za ndoa kutoka kwa waume zao
kwa muda mrefu, kutokana na ulevi wa gongo uliopindukia, zimemfadhaisha
Mbunge wao, Joseph Selasini (Chadema).
Mbunge huyo amefikia hatua ya kusema kuwa familia yake na wananchi wa huko, wamefadhaika na kuingiwa na wasiwasi kuwa huenda wenzi wao katika ndoa zao ikiwemo ya mbunge, si waaminifu.
Selasini alisema hayo jana, alipokuwa akiuliza swali kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambapo alisema ingawa hali hiyo imewafadhaisha, lakini alitetea utengenezaji wa pombe za kienyeji, ikiwemo pombe haramu ya gongo.
Katika utetezi huo, Selasini alitaka Serikali iangalie namna ya kusaidia uboreshwaji wa pombe za kienyeji, kwa kuwa kipato chake kimekuwa kikisaidia ada za watoto, kujikimu na kuongeza kipato cha familia.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema kwa namna Selasini anavyozungumza, huenda anatetea suala la kuhalalisha pombe haramu aina ya gongo, na kama ndio hiyo Serikali itaendelea kupiga vita utengenezaji na matumizi ya pombe hiyo kwa sababu viwango vyake havipimiki.
No comments
Post a Comment