MSHAMBULIAJI wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe, ametamka kuwa timu bora msimu huu ni Yanga kwani imeonyesha kiwango cha hali ya juu kwa mara ya kwanza tangu aanze kucheza soka.
Mwakingwe alisema ubora wa Yanga unatokana na jinsi ambavyo wamemudu kuwa na umoja kuanzia ngazi ya wanachama, mashabiki, viongozi, benchi la ufundi pamoja na wachezaji.
“Nazungumza kwa maendeleo ya soka na si kishabiki kwani Yanga wameonyesha ubora katika safu zao zote na ndiyo maana wamestahili kutwaa ubingwa msimu huu na hilo liwe funzo kwa timu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu Bara,” alisema
Mwakingwe ambaye amechezea Burkinafaso ya Ligi Daraja la Kwanza, alisema ubora wa mchezaji unaanzia nje ya uwanja ndipo matunda yake yanaweza kuwa faida kwa klabu yake pamoja na kuwafurahisha mashabiki na hilo Yanga walilibaini mapema ndio maana msimu huu wamefanikiwa kutamba.
Pia hakusita kuizungumzia timu yake ya zamani Simba, kuwa imekuja kuzinduka kwenye mechi nne za mwisho jambo ambalo linawaweka kwenye presha ya juu kusaka nafasi ya pili kitu ambacho si kizuri katika soka kwani bila shaka lawama haziwezi kukosekana.
“Naipenda Simba ni timu yangu lakini ukweli Yanga, wamefanya kitu cha mfano imekuwa supa kuliko timu zote zilizoshiriki Ligi msimu huu na kuwa mfano,” alisema Mwakingwe.
No comments
Post a Comment